Mar 14, 2015

UKIKUTWA NA TIKETI FEKI YA YANGA NA PLATINUM KESHO TAIFA, UMEKWISHA!

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
YANGA SC imeonya, atakayekamatwa na tiketi feki za mchezo wao na Platinum FC kesho ‘amekwisha’.
Yanga SC wanaikaribisha Platinum FC ya Zimbabwe kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
Na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro amesema wamechapisha tiketi za kiwango cha juu, ambazo si rahisi mtu ‘kufoji’ akapatia kila kitu.

“Sasa atakayethubutu kufoji na sisi tukamnasa kwa kweli amekwisha,”amesema. Muro amewaasa mashabiki kununua tiketi katika sehemu zilizotajwa, ili kuepuka kununua feki.
Kiingilio cha chini kitakuwa na Sh. 5,000 kwa jukwaa la viti vya rangi bluu na kijani, wakati katika jukwaa la viti vya Rangi Chungwa itakuwa Sh, 10,000, VIP C Sh. 20,000, VIP B Sh. 25,000, na VIP A Sh 30,000.
Muro amesema tiketi zimeanza kuuzwa leo asubuhi katika vituo vya Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Aidha, amesema magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya Uwanja siku ya Jumapili.
Yanga SC imefika hatua hii baada ya kuitoa BDF XI ya Botswana, wakati Platinum iliing’oa Sofapaka ya Kenya.

0 maoni:

Post a Comment