Mar 12, 2015

MATUMLA JR KUPIGANA NA MCHINA MACHI 27, AKISHINDA ATAPANDA ULINGO MMOJA NA MAYWEATHER, PACQUIAO MEI 2 LAS VEGAS

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
BONDIA Mohamed Matumla anatarajiwa kupanda ulingoni Machi 27, mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kupigana na Wang Xin Hua wa China.
Hilo litakuwa pambano la uzito wa Super Bantam, kuwania nafasi ya kugombea taji la dunia la WBF, Mei 2, mwaka huu mjini Las Vegas, Marekani siku ambayo Manny Pacquiao wa Ufilipino atapigana na Mmarekani Floyd Mayweather Jr.
Yaani mshindi wa pambano kati ya Matumla Jr na Xin Hua atapata tiketi ya kwenda kupigana katika pambano la utangulizi la Mayweather na Pacquiao Mei 2, Marekani. 

Pambano hilo litatanguliwa na mapambano kadhaa mengine, yenye mvuto, likiwemo kati ya Ashraf Suleiman wa Tanzania dhidi ya Mmarekani, Joseph Rabotte uzito wa juu taji la International WBF.
Mabondia wa Tanzania, Karama Nyilawila na Thomas Mashali watachapana katika pambano la uzito wa Super Middle kuwania taji la WBF Intercontinental, wakati Japhet Kaseba na Maada Maudo watachapana katika uzito wa Light Heavy kuwania ubingwa wa Taifa.    

0 maoni:

Post a Comment