Jan 29, 2015

MLIBERIA WA YANGA ATAKA APEWE MUDA TU, ANA UHAKIKA ATATUPIA TU NYAVUNI.



Mshambuliaji wa Yanga, Kpah Sherman, amewataka mashabiki na wanachama wa Yanga kutomkatia tamaa kutokana na ukame wa mabao na kusema wanatakiwa kuwa wavumilivu.

Nyota huyo wa zamani wa Cetinkaya ya nchini Cyprus, anaaminika kuwa na makeke pamoja na usumbufu kwa safu za ulinzi, lakini kikwazo kikubwa kwake ni kuweka mpira kimiani, hali ambayo na yeye anakiri kumkwaza.

Sherman amesema mashabiki wanatakiwa kumpa muda wa kutosha na kwamba ipo siku hali hiyo itaisha na atawapa furaha.

“Mimi mwenyewe sijui, ila naamini ni hali ya kawaida kwa kila mchezaji kumtokea. Unakuwa na nafasi ya kufunga lakini unashindwa kufanya hivyo, ila binafsi naamini ni hali ya kupita. Cha msingi ni mashabiki wetu kuwa na subira.”

Alipoulizwa kama ni kuchezeshwa nafasi ya fowadi badala ya nafasi yake ya zamani, winga kushoto, Sherman alisema: “Hapana, kwanza kupangwa nafasi flani ni matakwa ya mwalimu, kwa hiyo pengine ameona ninafaa zaidi kucheza kama mshambuliaji wa pili ndiyo maana bado ananipa nafasi mara kadhaa katika nafasi hiyo.”

0 maoni:

Post a Comment