Feb 11, 2015

ALICHOKISEMA KOPUNOVIC KUHUSU DANNY SSERUNKUMA


IMG_0522
KOCHA mkuu wa Simba SC, Goran Kopunovic anafurahishwa na kiwango cha mshambuliaji wake, Raia wa Uganda, Danny Sserunkuma ambaye siku za karibuni amekuwa na makali ya kufumania nyavu.
Sserunkuma alifunga bao moja katika ushindi wa Simba wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda fc huko Nangwanda Sijaona na mabao mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Ruvu uwanja wa Taifa.
“Danny ni mtu anayevutia, nilikutananaye kwa mara ya kwanza huko Zanzibar, nadhani kwa kiasi fulani alikuwa na kiwango cha chini, lakini sasa anakuja. Amesema Kopunovic.
“ Unajua nafasi anayocheza Danny ndio nilikuwa nacheza katika maisha yangu ya soka na nawaelewa vizuri washambuliaji, wakati wote kitu muhimu ni magoli. Danny ni mtu wa kigeni, ni mchezaji wa kimataifa, anatoka timu ya taifa ya Uganda, ana uzoefu wa kucheza nje ya Uganda, alicheza Kenya katika klabu ya Gor Mahia,kwahiyo ni mchezaji muhimu katika timu” Ameongeza Kopunovic.
Mserbia huyo alipoulizwa kuhusu mwenendo wa klabu yake katika mechi za ligi kuu Tanzania bara na anajisikiaje kupata matokeo yasiyoridhisha, amejibu:  “Siku zote nasema ukweli, siku zote kocha Goran anaangalia mechi ijayo, mimi ni mpaganaji ninayetafuta mafanikio ya timu. Simba ni timu kubwa, inaungwa mkono sana, ina mashabiki wengi, nina furaha sana kwasababu mashabiki wako upande wangu, ni watu muhimu sana”. Amesema Kopunovic.
Kumekuwa na madai kuwa wachezaji wa Tanzania wanashindwa kuwaelewa makocha wa Kizungu, lakini Kopunovic amesema wachezaji wa Simba wanamuelewa vizuri.
“Nadhani ndiyo, mara zote naongea na wachezaji wangu kabla na baada ya mechi, maswali yote nayaelekeza kwa wachezaji kuhusu mazoezi, mfumo wangu, falsafa yangu na mapaka sasa hakuna mtu anayeniambia kuwa kocha tuna matatizo, hiki sio kitu kizuri kwetu, hiki ni kigumu, nadhani tunaenda vizuri”.
Simba imeshuka dimbani mara 13, imeshinda 3, imetoa sare 8 na  imefungwa mechi 2 na kutokana na matokeo hayo ipo nafasi ya 9 nyuma ya Kagera Sugar, Coastal Union, Mtibwa Sugar na Ruvu Shootings.
Mwishoni mwa wiki hii, Simba wataikabili Polisi Morogoro katika mechi ya ligi kuu itayopigwa uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.

0 maoni:

Post a Comment