Na Bertha Lumala, Dar es salaam
Azam FC, mabingwa watetezi wa
ligi kuu ya Tanzania Bara wamefanikiwa kurejea kileleni mwa msimamo wa
ligi hiyo baada ya kuichapa Mtibwa Sugar mabao 5-2 kwenye Uwanja wa Azam
uliopo Chamazi, Mbande jijini hapa jioni hii.
Mabao mawili ya kiungo Frank Domayo na washambuliaji Kipre
Tchetche na Didier Kavambagu, aliyefunga moja, yamewapa uongozi wa ligi
hiyo Azam FC wakifikisha pointi 25 sawa na Yanga SC waliowafunga Mtibwa
Sugar FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini hapa Jumapili na kukaa
kileleni kwa muda, lakini wanalambalamba wanabebwa na tofauti nzuri ya
mabao ya kufunga na kufungwa.Mechi hiyo ya kipigo kikubwa kwa Mtibwa Sugar FC msimu huu na kipigo kikubwa zaidi cha ligi hiyo msimu huu, imeshuhudiwa na Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mholanzi Mart Nooij aliyekuwa Jukwaa Kuu la Uwanja wa Azam.
Kagera Sugar FC, timu ndugu na Mtibwa Suga FC, ilifungwa mabao 4-0 dhidi ya Azam FC kwenye uwanja huo huo msimu uliopita, kikiwa ni kipigo kikubwa kwa tmabingwa hao wa Kombe la Tusker 2008 katika miongo miwili iliyopita.
Timu hiyo inayomilikiwa na familia ya tajiri mkubwa nchini, Said Salum Bakhresa (SSB), imefunga mabao 22 na kufungwa 12 wakati Yanga SC wamefunga mabao 15 na kuruhusu nyavu zao kutikishwa mara saba. Timu zote mbili zimecheza mechi 13.
Dakika ya 19 tu ya mchezo, mshambuliaji Tchetche, anayetoka kwa mabaingwa wa Afrika mwaka huu, Ivory Coast, alifunga mlango wa mabao kwa wenyeji Azam FC akiuwahi mpira uliogonga mwamba kutokana na shuti la winga mpya na hatari Brianm Majwega.
Hilo lilikuwa bao la pili kwa Tchetche katika mechi mbili baada ya kufunga pia bao la kwanza katika sare yao ya 2-2 dhidi ya Polisi Moro mjini Morogoro Jumamosi.
Kwa bao hilo, Tchetche, mfungaji bora wa ligi kuu ya Bara msimu wa 2012/13 na mchezaji bora wa ligi hiyo msimu uliopita, akafikisha mabao matano ligi kuu ya Bara msimu huu sawa na Ame Ally Amour wa Mtibwa Sugar FC na Danny Mrwanda wa Yanga SC.
Dakika nne kabla ya nusu saa ya mchezo, kiungo Domayo aliyerejea uwanjani Januari baada ya kukaa nje kwa muda mrefu kutokana kufanyiwa upasuaji wa goti nchini Afrika Kusini mwaka jana, alipatia bao la pili Azam FC akimalizia pasi fupi ya winga ‘fundi’ Majwega iliyopenyezwa ndani ya boski.
Hilo ni bao la pili kwa Domayo baada ya kufunga pia bao pekee katika mechi yake ya kwanza ya ligi kuu akiwa na kikosi cha Mcameroon Jopseph Omog waliyoshinda 1-0 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa CCM Kambarge mjini Shinyanga Januari 17.
Domayo alikuwa na nafasi ya kufunga bao katika shambulizi kali la kwanza la Azam FC, lakini akapaisha. Ilikuwa mechi ya tatu ya ligi kuu kwa Domayo ndani ya kikosi cha Azam FC.
Katika dakika ya 34 Musa Nampaka alifumua shuti la kushtukiza na kuwapatia Mtibwa Sugar FC bao akiitendea haki pasi murua ya Mzanzibar Ally Shomari Sharrif. Hilo ni bao la kwanza kwa Nampaka msimu huu.
Kinara wa mabao Didier Kavumbagu alihakikisha anaendelea kuiwakimbia Samwel Kamuntu wa JKT Ruvu Stars na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar FC wenye mabao sita baada ya kuifungia Azam FC bao la tatu baada ya kupewa pasi safi na kiungo Salum Abobakar ‘Sure Boy’ dakika tano kabla ya mapumziko.
Kwa bao hilo, Mrundi huyo amefikisha mabao nane msimu huu ambayo ni sawa na mabao yote aliyoyafunga mfungaji bora wa ligi hiyo msimu uliopita, Mrundi mwenzake Amisi Tambwe katika raundi saba za awali msimu uliopita.
Tchetche amerejea tena kambani dakika ya nne kabla ya kipenga cha mwisho na kufikisha mabao sita ligi kuu msimu huu akiwakamata Mandawa, Ame na Kamuntu. Tchetche amemalizia krosi nzuri iliyomiminwa na beki wa pembeni Shomari Kapombe baada ya gonga gonga nyingi zilizofanywa na kikosi cha Azam kuanzia katikati ya uwanja.
Dakika mbili kabla ya saa ya mchezo, Domayo aliyejiunga na Azam FC muda mfupi baada ya kumalizika kwa msimu uliopita akitokea Yanga SC, alitupia bao la nne kwa timu yake, la pili kwake katika mechi ya leo na la tatu kwake msimu huu baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Mohamed kutokana na shambulizi kali la wanalambalamba.
Dakika 12 baada ya goli hilo, yaani katika dakika ya 70, Ame Ally Amour alifunga bao la pili kwa Mtibwa Sugar FC akimalizia kwa ufundi pasi maridhawa ya mtokeabenchini Abdallah Juma ambaye ulikuwa mpira wake wa kwanza tangu aingie uwanjani kuchukua nafasi ya mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Mussa Hassan ‘Mgosi’.
Vikosi vilikuwa;
Azam FC: Manula, Kapombe, Nyoni/ Bocco (dk.65), Moradi, Wawa, Bolou/ Mudathir Yahya (dk. 55), Tchetche, Domayo, Kavumbagu/ Mcha (dk.80), Sure Boy na Majwega.
Mtibwa Sugar SC: Said Mohamed, Andrew Vicent, Majaliwa Mbaga, Ally Lundenga/ Vicent Barnabas (dk. 46), Salim Mbonde, Shaban Nditi, Ramadhani Kichuya, Musa Nampaka, Ame Ally Amour, Henry Joseph/ Ally Shomari (dk.33) na Musa Hassan ‘Mgosi’/ Abdallah Juma (dk. 70).
0 maoni:
Post a Comment