*El-Merrikh kutua Dar kesho
Na Bertha Lumala, Dar es SalaamWakati wapinzani wa Azam FC katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, El-Merrikh FC ya Sudan watatua jijini Dar es Salaam kesho, Yanga SC wameahidi kuichakaza kwa pasi nyingi timu ya BDF XI ya Botswana katika mechi yao ya hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Azam FC (CEO), Saad Kawemba, kikosi cha El-Merrikh, mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Sudan, kitatua jijini hapa kesho tayari kwa mechi yao ya kwanza ya hatua ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi jijini hapa Jumapili.
MKWASA: TUTAICHAKAZA BDF
Kocha Msaidizi wa Yanga SC, CHarles Boniface Mkwasa amesema kikosi chao kitacheza soka la pasi nyingi lililopotea tangu kufukuzwa kwa Mbrazil Marcio Maximo, ili kukikarisha kikosi cha BDF XI ya Botswana katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mechi hiyo itachezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa jijini hapa kuanzia saa 10:00 jioni.
Kuelekea mechi hiyo, Mkwasa amesema: “BDF XI ni timu ya jeshi, tunatambua kwamba itacheza soka la kutumia nguvu nyingi kama ilivyo kwa timu za majeshi za hapa nchini.”
“Tunatambua watacheza soka la namna hiyo, hivyo tumejipanga kuwadhibiti kwa kucheza pasi nyingi ili tuwafunike na kuwachosha maana watakuwa wakiutafuta mpira,” amesema zaidi kocha huyo wa zamani wa Twiga Stars na Ruivu Shooting, anayesifika kwa kufundisha soka la kasi na la pasi fupi fupi.
Tayari Yanga SC imeshatangaza viingilio vya mechi hiyo, kiingilio cha chini kiwa Sh. 5,000.
0 maoni:
Post a Comment