Feb 14, 2015

OKWI NTAKOMAA NA YANGA MPAKA KIELEWEKE



Baada ya kipa Juma Kaseja kufikishwa mahakamani na Klabu ya Yanga kwa madai ya kuvunja mkataba na klabu hiyo, mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi amesisitiza kuwa atapambana mpaka mwisho na Yanga ili wamlipe haki yake anayoidai.

Okwi, kupitia Kampuni ya Agaba Muhairwe & Co Advocates ya Kampala, Uganda, alifungua kesi hivi karibuni dhidi ya Yanga akiidai klabu hiyo dola 62,000 (Sh milioni 107) kwa madai ya kukiuka mkataba aliokuwa amesaini na klabu hiyo, madai ambayo yameshafika kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Okwi amesema kuwa awali aliwaandikia barua Yanga kuhusu madai yake hayo ikiwa ni fedha za makubaliano ya usajili ambazo hawajammalizia, lakini uongozi huo ulikaa kimya.
Anasema baada ya hapo akaandika barua nyingine ya kuwakumbusha juu ya madai hayo yaliyotokana na hukumu ya Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Mchezaji huyo raia wa Uganda aliongeza kuwa kutokana na hali ya kuonyesha kupuuza jambo hilo, sasa yupo kwenye hatua mpya ya kuwaandikia barua nyingine itakayokuwa na shinikizo la kulipwa mara moja, la sivyo atapeleka shitaka lake mbele zaidi.
“Nipo katika mchakato wa kuona nifanye nini na mwanasheria wangu baada ya barua za awali kutojibiwa, nimesikia kutoka kwao kuwa wamekata rufaa juu ya ile barua yangu na kutaka kunishtaki Fifa bila ya kunitaarifu kwa kunipa barua juu ya kile kinachoendelea.
“Nitatoa shinikizo la kulipwa ndani ya muda fulani. Wasipofanya hivyo nitapeleka shitaka langu ngazi za juu zaidi,” alisema Okwi.

0 maoni:

Post a Comment