Mar 4, 2015

MAKOMBE 15 MIKONONI MWA TERRY, ANASUBIRI LA 16

Na Saleh Ally
OKTOBA 28, 1998 beki John Terry akiwa kinda aliingia uwanjani kuichezea Chelsea mechi yake ya kwanza ikipambana na Aston Villa katika mechi ya Kombe la Ligi.

Miaka 10 baadaye, ilikuwa 2008, Terry akawa adui baada ya kuteleza na kukosa penalti ya mwisho katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mjini Moscow, Urusi dhidi ya Manchester United.
Maisha yanasonga, mengi yanapita lakini kibaya kinaweza kubadilika na kuwa kizuri kama mhusika anajitambua. Hakuna anayeweza kukataa kwamba kweli Terry maarufu kama JT sasa ni shujaa wa Chelsea.
Beki ambaye atakumbukwa, nahodha ambaye atakuwa gumzo kwa kipindi kirefu baada ya kustaafu. Sasa anasonga ukiongoni akiwa na miaka 34, lakini anaendelea kuibebesha Chelsea vikombe na mikono yake ndiyo mpokeaji mkuu.

Alianza kujihakikishia namba katika kikosi cha Chelsea katika msimu wa 2000-01, alipocheza mechi 23 zote akianza. Msimu uliofuata akawa tegemeo akishirikiana na Marcel Desailly na Desemba 5, 2001, rasmi akakabidhiwa unahodha.
Miaka 14 sasa tokea amekuwa nahodha wa kikosi cha Chelsea, tayari JT ana makombe 14 mkononi mwaka aliyoshinda akiwa na klabu yake hiyo ya Chelsea.
Hauwezi ukamzungumzia JT bila ya utukutu na kashfa lukuki, mwaka 2002 akizichapa na baunsa, wakamchangia na mwisho akapandishwa kizimbani. Miezi michache baadaye akakutana na kashfa nyingine ya kumdhalilisha mtalii wa Kimarekani, ikawa kesi nyingine.

Usisahau, JT aliingia katika kashfa ya kutembea na mpenzi wa mshikaji wake kitambo, beki Wayne Bridge. Hiyo haitoshi, akambagua Anton Ferdinand na kusababisha ugomvi mkubwa kati yake na aliyekuwa mshikaji wake, Rio Ferdinand.
Kwa kifupi, JT ni mtukutu hasa lakini unaporudi kazini, JT ni kati ya mabeki bora zaidi England hadi msimu huu kwa kuwa Chelsea inapambana kupata ubingwa wa Ligi Kuu England na kama itashinda, atakuwa amebeba kombe la 16.
Maana yake JT tayari ameweka rekodi mpya katika mikono yake ya unahodha wa miaka 14 na makombe 15 aliyoyashika.

Nani anaweza kusema JT hajitumi, si mbunifu au si makini? Ubora wa kazi zake unafuta makosa na utukutu wake wote na ndivyo binadamu wanavyoishi, kwamba wakati mwingine vizuri kuangalia katika mazuri ya mtu kuliko kujali zaidi makosa.
Makombe la Ligi ya Mabingwa, Europa, Ligi Kuu England, FA, Kombe la Ligi na mengine. Mchezaji yupi wa nyumbani Tanzania anawaza atakuwa amefanya nini wakati soka lake litakapokuwa limefikia ukingoni?
Inawezekana kukawa na tofauti kubwa kati ya Ibrahim Ajibu wa Simba na JT. Kweli kinda huyo wa Simba, ndoto yake kuwa na gari kali ikiwezekana nyumba pia, lakini mafanikio makubwa yanajenga kila kitu na gari na nyumba, zenyewe zinamfuata, tena anachagua.
Mchezaji yupi kinda au anayefanya vizuri wa Yanga, Azam FC, Coastal Union na kwingine anayeamini kama mafanikio hayajakaa vizuri katika timu anayochezea, anaweza kutoka nje ya Tanzania na kubadilisha mambo? Alipo, ndipo alipo na amefika! Vipi atafikia alipofikia JT?
Wachezaji nao ni mashabiki, kazi yao kusifia vinavyofanywa na wenzao wakati wao hawafanyi lolote. JT angeweza kufanya hivyo, lakini hawezi kwa kuwa alikuwa anataka kufanya zaidi ya alivyotaka kufanya. JT tayari ana makombe hayo 15, anatafuta la 16. Wewe je?
MAKOMBE NA KLABU:
3 – Ligi Kuu England: 2004–05, 2005–06, 2009–10
5 - FA Cup: 1999–00, 2006–07, 2008–09, 2009–10, 2011–12
3 – Kombe la Ligi: 2004–05, 2006–07, 2014–15
1 – Ligi ya Mabingwa Ulaya: 2011–12
1 - Europa League: 2012–13
2 – Ngao ya Jamii: 2005, 2009
VIKOMBE BINAFSI:
1 – Mchezaji wa mwaka wa PFA: 2004–05
3 – Mchezaji katika kikosi cha mwaka cha PFA: 2003–04, 2004–05, 2005–06
2 – Mchezaji wa mwaka Chelsea: 2001, 2006
1 – Ndani ya kikosi Bora cha Kombe la Dunia: 2006
5 – Mchezaji bora wa FIFPro World XI: 2005, 2006, 2007, 2008, 2009
3 – Beki bora wa klabu wa UEFA: 2005, 2008, 2009

4 – Timu bora ya mwaka ya UEFA: 2005, 2007, 2008, 2009

0 maoni:

Post a Comment