Mar 4, 2015

SIMBA YAMFUKUZIA NDUGU YAKE TWITE

MBUYU (KUSHOTO) NA KABANGE WAKATI WAKIICHEZEA APR YA RWANDA.
Jina la nahodha na kiungo mkabaji wa FC Lupopo ya Kongo, Kabange Twite, limetajwa kwenye orodha ya wachezaji anaowataka Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia, Goran Kopunovic, kwenye usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.


Awali, kiungo huyo ambaye ni pacha wa kiraka wa Yanga, Mbuyu Twite, alitakiwa kutua Jangwani misimu miwili iliyopita ya Ligi Kuu Bara.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya kamati ya usajili ya timu hiyo, kocha huyo Mserbia ndiye ametoa mapendekezo ya  uongozi kuhakikisha wanamsajili kiungo huyo msimu ujao.

Chanzo hicho kilisema, kocha huyo hivi sasa yupo kwenye mazungumzo ya awali na Kabange anayemudu kucheza namba sita inayochezwa na Jonas Mkude ndani ya uwanja.

“Kocha ametoa mapendekezo ya kumsajili Kabange kutokana na kumjua akiwa anaifundisha Polisi Rwanda na kiungo akiwa anaichezea APR ya inayoshiriki Ligi Kuu ya Rwanda.

“Hivyo kocha huyo anaendelea na mazungumzo na kiungo huyo kwa ajili ya kumsajili katika msimu ujao, atamsajili Kabange baada ya kuona upungufu kwenye kikosi chake kwenye safu hiyo ya kiungo,”kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa pacha wa mchezaji huyo Mbuyu kuzungumzia hilo alisema kuwa “Ni kweli kabisa yapo mazungumzo ya awali yanayoendelea kati ya Kabange na kocha wa Simba kwa ajili ya kuja kuichezea timu hiyo.


“Asilimia ni kubwa ya Kabange kutua kuichezea Simba, kwa sababu huyo kocha mpya wa Simba anamjua vizuri Kabange, aliwahi kuifundisha Polisi Rwanda, hivyo anaujua vizuri uwezo wa Kabange,”alisema Twite.

0 maoni:

Post a Comment