Feb 4, 2015

YANGA YAKAA KILELENI

Na Mahmoud Zubeiry, TANGA
YANGA SC imepanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Shujaa wa pointi tatu za Yanga SC leo ni Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’, aliyefunga bao hilo pekee mapema tu kipindi cha kwanza, baada ya kupanda kwenda kusaidia mashambulizi. 
 
Yanga SC sasa inatimiza pointi 22 baada ya kucheza mechi 12, moja zaidi ya mabingwa watetezi, Azam FC walioteremkea nafasi ya pili kwa pointi zao 21.
Ilikuwa ni dakika ya 12 ya mchezo, wakati Cannavaro alipomalizia kwa kichwa mpira uliounganishwa kwa kichwa pia na mshambuliaji Mliberia Kpah Sherman kufuatia mpira wa kurushwa wa beki Mbuyu Twite.
Nadir Haroub 'Cannavaro ' akishangilia baada ya kuifungia bao pekee Yanga SC Mkwakwani leo. Kushoto ni kipa Shaaban Kado akiwa ameduwaa

Timu hizo zilishambuliana kwa zamu na hakukuwa na burudani, zaidi ya ‘butua butua’, kushindana nguvu na kasi, kutokana na timu zote kuhofia kucheza ‘kandanda ya kitabuni’ kwa sababu ya hali mbaya ya Uwanja wa Mkwakwani.
Kipindi cha pili, Yanga SC walianza kucheza kwa kujihami kulinda bao lao, huku wakifanya mashambulizi machache ya kushitukiza.
Coastal Union ilikaribia kusawazisha bao dakika ya 82 baada ya Godfrey Wambura kumpa pasi nzuri, Hussein Sued, ambaye licha ya mabeki wa Yanga kumuacha wakidhani ameotea, lakini akapiga nje akiwa ndani ya sita.
Winga wa Yanga SC, Simon Msuva akitafuta maarifa ya kumtoka beki wa Coastal, Sabri Rashid
Kipa wa Coastal, Shaaban Kado akiokoa moja ya hatari langoni mwake leo
Mshambuliaji wa Yanga SC, Kpah Sherman (kushoto) akipambana na beki wa Coastal, Abdallah Mfuko kulia

Kwa ujumla mchezo ulikuwa wa ‘kindava ndava’ na hakukuwa na burudani yoyote- na sifa ziwaendee marefa wa mchezo wa leo kwa kuumudu vyema.
Kipindi cha kwanza mashabiki wa Coastal waliwavurumushia mvua ya mawe mashabiki wa Yanga, hadi Polisi wakaenda kuwasaidia.
Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Shaaban Kado, Mbwana Hamisi, Sabri Rashid, Abdallah Mfuko, Juma Lui, Abdulhalim Humud, Joseph Mahundi/Said Mtindi dk60, Godfrey Wambura, Hussein Sued, Rama Salim na Itubu Imbem. 
Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Rajab Zahir, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela, Simon Msuva, Said Juma ‘Kizota’, Kpah Sherman, Amisi Tambwe/Danny Mrwanda dk83 na Andrey Coutinho/Hussein Javu dk65.

0 maoni:

Post a Comment