Feb 4, 2015

YANGA YAMGEUKA MRISHO NGASSA

 
Uongozi wa Klabu ya Yanga umefunguka kuwa hauhusiki na deni la mshambuliaji wao, Mrisho Ngassa anayedaiwa fedha na Benki ya CRDB kwa kuwa yeye aliomba udhamini katika timu hiyo na si kulipiwa kama anavyodai.

Hivi karibuni, Ngassa alinukuliwa akidai kushindwa kuwa katika kiwango kizuri cha kuitumikia timu yake hiyo kufuatia deni la shilingi milioni 45 alizokopa CRDB kwa ajili ya kuilipa Simba ili ajiunge na Yanga, baada ya kusaini timu mbili kwa madai kuwa uongozi wa timu hiyo ungemsaidia laki tano kila mwezi.

Msemaji wa Yanga, Jerry Muro, alifunguka kuwa Yanga haikuwa na mkataba wa makubaliano na Ngassa wa kumsaidia kumlipia kwa kuwa klabu hiyo ilikubali kumdhamini katika Benki ya CRDB kama mwajiriwa wake tu.

“Ieleweke kuwa Yanga ilimdhamini Ngassa wakati alipokwenda kukopa fedha CRDB kwa ajili ya kulipia deni lake na tulifanya hivyo kama waajiri wake, lakini hakukuwa na makubaliano ya kuweza kumsaidia katika kulipa deni hilo.

“Siku zote taratibu za kukopa zinakuwa kati ya benki na mkopaji na wala hatuhusiki na sisi tulimdhamini tu katika kukamilisha ukopaji wake kwani deni alilokopa ni yeye na CRDB na si Yanga, naomba watu waelewe hivyo,” alisema Muro.

0 maoni:

Post a Comment