KILA la kheri Azam fc katika mechi yenu ya raundi ya kwanza ya ligi ya mabingwa barani Afrika dhidi ya El Merreick ya Sudan inayopigwa leo jioni uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Ili kusaka ushindi katika mechi hiyo Mliweka kambi ya wiki mbili nchini Uganda, Mkashiriki michuano ya kombe la Mapinduzi na mkaenda kukaa DR Congo kwa wiki moja kushiriki kombe la Mazembe.
Hayo ni maandalizi makubwa kwenu ninyi na leo Watanzania wapo nyuma yenu kuona mtavuna nini.
Sehemu zote mlizoweka kambi na kushiriki michuano hamkufanya vizuri, timu haikuonekana kucheza kwa kiwango cha juu, lakini haitoshi kujenga imani kuwa leo hamtafanya vizuri.
Merreick waliwatoa robo fainali ya kombe la Kagame kwa mikwaju ya penalti mwaka jana na kuwarudisha Dar, leo mnakutana nao katika michuano mikubwa zaidi ya klabu bingwa Afrika.
Wasudan hao ni miongoni mwa timu bora na zenye uzoefu wa michuano hii ambayo Azam fc mnashiriki kwa mara ya kwanza. Kutokana na hili lazima muingie uwanjani na tahadhari kubwa ili kutowaruhusu kupata goli la ugenini.
Michuano hii inahitaji nidhamu ya mchezo hasa unapokuwa uwanja wa nyumbani. Kinachotakiwa ni kuhakikisha unapata ushindi wa zaidi ya mabao 3-0 uwanja wa nyumbani na ukishindwa sana basi ushindi 2-0.
Hii itakusaidia kujiamini zaidi ugenini kwani kazi yako kubwa itakuwa ni kulinda ushindi huo na unaweza kuingia na mbinu ya kujilinda na kutengeneza mashambulizi ya kushitukiza.
Ingawa mfumo huu ni hatari kwani unawakaribisha zaidi wapinzani langoni kwako na kwa kuwa mpira wa miguu ni mchezo wa makosa, unaweza kuruhusu mabao.
Najua kocha wa Azam fc, Mcameroon, Joseph Marius Omog atatumia mbinu ya kushambulia sana kwasababu anahitaji ushindi nyumbani, sio jambo baya, lakini nidhamu ya ulinzi kuanzia safu ya kiungo na ulinzi lazima iwe kubwa.
Merreick watacheza mpira wa polepole na kujaribu kuwatuliza Azam fc watakuwa na kasi, kinachotakiwa kufanyika ni Azam kucheza kwa kasi na kushambulia zaidi.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Azam fc!!
0 maoni:
Post a Comment