Feb 15, 2015

YANGA SAFARI MBEYA MECHI MBILI DABO

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KIKOSI cha Yanga SC kinaondoka Alfajiri ya kesho Dar es Salaam kwa basi lao kubwa, kuelekea Mbeya kwa ajili ya mechi na wenyeji Prisons Alhamisi.
Yanga SC watateremka Uwanja wa Sokoine, Mbeya katikati ya wiki kusaka pointi tatu dhidi ya timu hiyo ngumu inayomilikiwa na jeshi la Magereza katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Baada ya mchezo huo, Yanga SC watashuka tena Uwanja wa Sokoine kumenyana na wenyeji wengine, Mbeya City Jumapili katika mfululizo wa ligi hiyo. 

Yanga SC wanakwenda Mbeya, wakitoka kuanza vizuri mechi ya kwanza Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuifunga BDF XI ya Botswana mabao 2-0 jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na wakitoka Mbeya tu, wataunganisha safari hadi Gaborone kwa ajili ya mchezo wa marudiano na BDF. 
Kocha wa Yanga SC, Mholanzi Hans van der Pluijm bado na mtihani wa kufanyia kazi mapungufu ya safu yake ya ushambuliaji ambayo inashindwa kutumia nafasi nyingi inazotengeneza.

0 maoni:

Post a Comment