Feb 15, 2015

MCHEZAJI WA KITANZANIA APATA TUZO QATAR

TANGAZI 3
Kinda Martin Tangazi ambaye amenyakua tuzo ya mchezaji bora wa Aspire Sports Academy ya nchini Qatar kwa mwezi Januari.
Na. Richard Bakana, Dar es salaam
Mvua ya Neema imezidi kumyeshea Kinda wa Kitanzania, Martin Tangazi anayekipiga kunako Academy ya Aspire nchini Qatar baada ya juzi Ijumaa Februari 13, kufanikiwa kuwaburuza Waarabu, Waivory Coast, Wanigeria na Waghana na kujinyakulia tuzo ya mchezaji Bora wa Academy.
Akizungumza na Shaffihdauda.com  akiwa Qatar, Tangazi ambaye aliondoka nchini enzi za utwala wa Leodegar Tenga, mwaka 2013, amesema kuwa haikuwa vyepesi kwake kuchukua tuzo hiyo ya mwezi Januari kufatia upinzani mkali uliopo ndani ya Academy yao ambayo imejaa vipaji lukuki kutoka kila kona ya Dunia hususani Mataifa ya Afrika.
“Kila mwezi lazima achaguliwe mchezaji bora wa Academy nzima, wachezaji wote wanampigia kura mtu wanaye muona anajua zaidi ya wenzake, wote tunavipaji, lakini jitihada zangu binafsi ndio zimeweza kufanikisha mimi kuchukua tuzo hii ambayo huwa ni heshima kubwa sana mchezaji akiipata” Amesema Tangazi ambaye amefikisha tuzo mbili mfululizo baada ya mwezi Desemba 2014 kuichukua kwa mara ya kwanza.
Tangazi amewataja wapinzani wake katika kinyang’anyilo hicho kuwa walikuwa ni Kalamo Ceesy, raia wa Ivory Coast, Yahuza Idris ambaye ni raia wa Nigeria, Emanuel Asuquo wa Ghana, Coulibay Joseph ambaye pia anatoka Ivory Coast pamoja na yeye mwenye kutoka Tanzania, Watano hao ndio waliingia top 5 ambayo pia ilichujwa na kupata nyota watatu ambao mwisho wa siku Kijana huyo mwenyeji wa Mkoa wa Morogoro akaibuka mshindi.
“Zilipigwa kura na wachezaji wenzetu, Mimi na wenzangu wawil ambao ni Yahuza Idris na Emanuel Asuquo ndIyo tulifanikiwa kuingia fainali” Amesema Tangazi ambaye toka ajiunge na Academy hiyo alikuwa akishika nafasi ya pili naya tatu.
Kinda huyo ambaye yupo kwenye kikosi cha U17 cha Aspire Sports Academy, amesema kuwa jumla ya kura 95 zilipigwa kwa watatu hao likini yeye ndiye akaibuka kidedea kwa kuvuna pointi 40, huku  Emanuel Asuquo  raia wa Ghana akiibuka mshindi wa pili kwa pointi 32 na Mnigeria Yahuza Idris akiwa katika nafasi ya tatu akiambulia alama 23.TAGAZI-5
Tangazi amesema kuwa ujio wa  tuzo hiyo kwake ni kama kufunguliwa mlango wa kujituma zaidi ili aweze kutimiza ndoto zake za kutaka kuitikisa Dunia kama ilivyo kwa Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Lionel Messi wa Barcelona.
“Dah!  Nilikuwa naambulia nafasi ya pili na tatu tu lakini nimefurahi Sana, hii imenipa changamoto zaidi ya kuongeza juhudi zaidi ili niweze kutimiza ndoto zangu” Amesema Tangazi ambaye anamkubali sana Mtanzania mwenzake Mbwana Samatta kutokana na kazi anayoionyesha akiwa TP Mazembe.
Mchezaji huyo wa zamani wa Twalipo Camp ya Jijini Dar es salaam, amesema kuwa Tanzania kuna vipaji vingi sana huku akitoa ushauri kwa vijana kujituma na kusimamia ndoto wanazo jiweke katika maisha.
“Kwanza nakubali Tanzania tuna vipaji vingi sana na tunaweza kupambana, Napenda kuwaambia vijana wenzangu kuwa wajitume sana, hiyo pekee ndio siraha ya maisha” Amemalizia Nyota huyo wa Kesho wa Taifa Stars na Dunia.

0 maoni:

Post a Comment