Feb 7, 2015

HUU NDIO UBABE WA COSTA NA TERRY UWANJANI

Na Saleh Ally
TABIA za beki mkongwe wa Chelsea, John Terry, ni kupenda kujitambulisha kwa washambuliaji anaokutana nao wakati timu yake ikiwa uwanjani.
Terry, maarufu kama JT, hajitambulishi kwa kupeana mikono, badala yake maneno ya kibabe au kumgongagonga mshambuliaji anayekuwa anamkaba ili kumuonyesha siku hiyo shughuli ni pevu.

Nahodha huyo wa Chelsea amekuwa akifanya hivyo mara nyingi ikionekana kutaka kumtawala mapema kabisa kisaikolojia mshambuliaji anayemkaba kwamba ajue amekutana na kiboko yake au beki katili na asiyetaka mchezo na kazi yake.
Wakati akiwa Liverpool, mshambuliaji Fernando Torres aliwahi kusema kila walipokutana na Chelsea alifanya juhudi kubwa kuhakikisha anafunga kwa kuwa alitaka kumuonyesha Terry ambaye hakufurahishwa na ubabe wake mara kwa mara.
Huenda mara kadhaa, Terry amekuwa akibadili mbinu zake, lakini hiyo ni moja ya kubwa alizonazo. Wakati fulani, mpango huo wa Terry ulifeli.

Katika mechi ya kwanza ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atletico Madrid, Terry alianza mapema mipango yake ya kutaka kumuonyesha mshambuliaji Diego Costa kwamba yeye ni nani. Lakini majibu yalikuwa makali kuliko alivyotegemea na ndipo akagundua kuwa Costa ni namba nyingine na huenda mfumo alioutumia kwa mara ya kwanza haukuwa sahihi.
Kitendo cha Costa kuwakanyaga mabeki Emre Can na Martin Skrtel wa Liverpool kimewafanya wengi waamshe mjadala wa mshambuliaji huyo raia wa Hispania mwenye asili ya Brazil.
Maswali yamekuwa ni mengi, kama kweli anafaa kuichezea Chelsea, kama kweli wanastahili kuwa na mchezaji mkatili hivyo. Mwisho wengi wanahoji vipi awe mjeuri namna hiyo? Ingawa wanavutiwa na uwezo wa kazi zake maana ndiye anaongozwa kwa kutikisa nyavu katika Ligi Kuu England.
Costa ni mtoto wa Uswahilini, amekulia maisha hayo na hakuwahi kuishi maisha ya mafunzo ya soccer kwenye ‘academy’ kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa Ulaya.
Ubabe wa mechi za mchangani ambazo alikuwa maarufu sana, bado uko kwenye damu yake, ndiyo maana anawapa tabu sana Wazungu.
Costa alizaliwa katika mji mdogo wa Lagarto katika Jimbo la Sergipe nchini Brazil. Miaka yote alikuwa akicheza soka la mchangani na alikuwa maarufu sana.
Hadi alipofikisha miaka 16, ndiyo alichukuliwa hadi jijini Sao Paulo na kujiunga na timu iliyokuwa na mafunzo sahihi ya mchezo wa soka.
Waliocheza naye soka katika Mji wa Lagarto kabla hajaondoka kwenda Sao Paulo, wanasema alikuwa mjeuri, mtu mwenye hasira na hakuwa na woga hata kidogo.
Lakini kituko cha kumpiga mchezaji halafu akakimbilia kumsukuma na kumghasi mwamuzi kilikuwa maarufu zaidi. Baadaye Costa alifungiwa miezi minne. Wakati huo alikuwa akiichezea Barcelona Esportiva Capella.
Aliwahi kubatizwa jina la Picardia, neno hilo la Kihispania lenye maana ya mpiganaji au mtu asiye na hofu na ndivyo anavyoonekana.
Hii inaonyesha kiasi gani uchezaji wa kibabe Costa hautakwisha na ataendelea kuwa namna hiyo kwa kuwa hakucheza soka la mafunzo linalomuonyesha afanye vipi kuonekana ni mwenye nidhamu.
Takwimu zinaonyesha hata kabla ya msimu kwisha, ameshasababisha tafrani za kawaida mara 22, amekwidana na mabeki mara tano, amewasukuma kwa kifua mara 13, amewasukuma kwa mikono mara 15 na amekutana na mabeki uso kwa uso na kutoa maneno ya kibabe mara 11.
Pamoja na kwamba ameshakutana na adhabu kutoka FA, lakini haimbadilishi yeye kuwa alivyo na wengi wamekuwa wakisema ni zawadi nzuri kwa mabeki wa England ambao wengi wamekuwa wababe kwa washambuliaji.
 Mara kadhaa, Costa ameonekana akiwa amechaniwa jezi au bukta. Lakini amekuwa akionyesha sehemu alizoumizwa na viatu vyenye njumu za chuma za mabeki hao ambao sasa wameanza kulalamika.
Hakuna ubishi tena unaweza kusema ubabe wa Costa ni dawa ya mabeki wababe wa England na karibu kila mchezo amekuwa akizozana nao na mara nyingi kuwafanya wadau wa soka kuwaonea huruma mabeki.
Kwa zaidi ya miaka 20, hakuna aliyewahi kulalamika mabeki wa Ligi Kuu England wamekuwa wakionewa hadi Costa alipotua England. Je, ataendelea hivyo hadi mwisho?
Mabao anayofunga anaonyesha ana uwezo na hilo alilidhihirisha Hispania kabla ya kutua England. Je, kuna mengi anafunga baada ya kuwatisha mabeki?
Jiulize, mabeki wa England hasa wale wa kati ambao wengi ni wakatili, wataendelea kumvumilia na kushitaki bila ya kumtafutia dawa?
Ila ukweli, mtoto wa Uswahilini anawapa shughuli mabeki hao licha ya wao kutamba kwamba England ndiyo kwa wababe.
Kwa sasa Costa ni kati ya burudani zinazovutia zaidi katika soka England. Kila anapokuwa anaitumikia Chelsea, wengi hupenda kuona anavyofunga na sasa imegeuka, wengi wanapenda kuona anavyopambana na mabeki wababe.

0 maoni:

Post a Comment