Feb 7, 2015

YANGA SC KUWEKA KAMBI JESHINI

YANGA SC imefuta mpango wa kwenda kuweka kambi Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya BDF XI ya Botswana.
Sasa, vigogo hao wa soka Tanzania wataingia kambini Jumatatu katika hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani, 

Dar es Salaam kwa maandalizi ya mchezo huo, unaosubiriwa kwa hamu na mashabiki wake.
Na timu hiyo inayofundishwa na Mholanzi, Mart Nooij anayesaidiwa na Mzalendo, Charles Boniface Mkwasa itakuwa ikifanya mazoezi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki yote kuelekea mchezo huo.
Hatua hiyo inafuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukataa ombi la Yanga SC kutaka mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Mtibwa Sugar uahirishwe ili wapate fursa nzuri ya maandalizi ya mchezo wao na BDF XI.
 
Baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Jumatano, Yanga SC iliondoka asubuhi ya Alhamisi kwenda kuweka kambi Bagamoyo kuendelea na maandalizi ya mchezo mwingine wa ligi hiyo, dhidi ya Mtibwa Sugar.
 
Yanga SC watacheza mechi ya tatu ndani ya wiki moja kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya mabingwa wenzao wa zamani wa Ligi Kuu, baada ya Jumapili iliyopita kulazimishwa sare ya 0-0 na Ndanda FC na Jumatano kushinda 1-0 dhidi ya Coastal Union. 
Yanga SC ilipanda kileleni mwa Ligi Kuu katikati ya wiki kufuatia ushindi huo wa ugenini, Tanga kwa kutimiza pointi 22 baada ya kucheza mechi 12, moja zaidi ya mabingwa watetezi, Azam FC walioteremkea nafasi ya pili kwa pointi zao 21.
 
Shujaa wa pointi tatu za Yanga SC siku hiyo alikuwa ni Nahodha Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’, aliyefunga bao hilo pekee mapema tu kipindi cha kwanza, baada ya kupanda kwenda kusaidia mashambulizi. 
Ilikuwa ni dakika ya 12 ya mchezo, wakati Cannavaro alipomalizia kwa kichwa mpira mpira wa kurushwa wa beki Mbuyu Twite na kuipandisha kileleni Yanga SC. 

0 maoni:

Post a Comment