Feb 7, 2015

LEO DERBY KATIKA MAJIJI YA LIVERPOOL, LONDON

LONDON, England
UTAMU wa soka la Ulaya utaendelea wikiendi hii. Vita ya kusaka ubingwa wa England nayo itazidi kupamba moto katika mechi za leo na kesho, lakini kubwa zaidi linalozungumzwa kitaa ni ‘derby’ (mechi zinazohusisha timu zinazotoka mji mmoja) mbili kubwa nchini England.

Derby ya kwanza inatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa White Hart Lane ambayo itazikutanisha timu zinazotokea katika Jiji la London, yaani Tottenham Hotspur dhidi ya Arsenal katika mtanange wa kukata na shoka utakaochezwa kuanzia saa 9:45 alasiri.

Lakini baadaye saa 2:30 usiku, kutakuwa na derby nyingine itakayozikutanisha timu zinazotokea jijini Liverpool, yaani Everton na Liverpool FC ambazo zitapambana vikali kwenye Uwanja wa Goodison Park.
Tottenham vs Arsenal
Vita hii inasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka sehemu mbalimbali duniani. Mechi itachezeshwa na mwamuzi mkongwe, Martin Atkinson, raia wa England.

Utamu wa mechi hii unatokana na timu zote kuwa kwenye kiwango bora katika mechi zake za hivi karibuni. Katika michezo yao mitano iliyopita, Tottenham wameshinda mitatu, wametoa sare mmoja na kupoteza mmoja, wakati Arsenal wenyewe wameshinda michezo yao yote mitano iliyopita.
Katika michezo yao mitano iliyopita waliyokutana, Arsenal imeshinda mara tatu, wakati Spurs imeshinda mara moja tu huku zikitoka sare mara moja.

Hata hivyo, pamoja na Arsenal kushinda mara nyingi dhidi ya wapinzani wao hao katika siku za hivi karibuni, bado mpambano unatarajiwa kutotabirika kutokana na kiwango cha sasa cha Spurs ambayo inawategemea zaidi washambuliaji wake Harry Kane na Christian Eriksen walio kwenye ‘fomu’ kwa sasa.

Supastaa wa Arsenal, Mchile, Alexis Sanchez, anatarajiwa kuukosa mchezo huo wa leo kutokana na kuendelea kusumbuliwa na majeraha ya nyama za paja yaliyomuweka nje ya uwanja katika ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Aston Villa wiki iliyopita, lakini kocha Arsene Wenger atashusha pumzi kufuatia kurejea kwa mpachika mabao wake, Danny Welbeck.
Timu zote hizi, zipo katika mapambano ya kuhakikisha zinakuwemo ndani ya nne bora ili zipate nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Kama Arsenal iliyo katika nafasi ya tano ikishinda kwenye mtanange huu, itakuwa imeingia hadi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa England kwa kuwa itakuwa imebakiza pointi nane tu iwafikie vinara Chelsea ambao baadaye watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Aston Villa. Lakini Spurs ikifungwa itakuwa inazidi kujiweka pabaya katika vita ya kuingia ‘top 4’.

Kama Spurs iliyo katika nafasi ya sita ikishinda mchezo huo, itaipiku Arsenal kwenye nafasi ya tano na inaweza ikaingia moja kwa moja ndani ya nne bora na kusubiri matokeo ya Southampton ambayo itakuwa mgeni wa QPR baadaye jioni.

Liverpool vs Everton:
Huu ni mtanange mwingine ambao umeshaanza kuwa gumzo mjini. Liverpool iliyo nafasi ya saba, iliuanza msimu huu kwa kusuasua kutokana na kuonekana kummisi mpachika mabao wao aliyeondoka, Luis Suarez, lakini sasa inaonekana kuanza kuimarika, hasa kutokana na ubora unaoonyeshwa na viungo wawili wa timu hiyo, Raheem Sterling na Philippe Coutinho.

Kwa upande wa Everton wanaonekana kutokuwa sawa msimu huu, kwani wameshindwa kuonyesha makali yao ya msimu uliopita ambapo walikuwa wanapigania kuingia kwenye ‘top 4’.
Everton wapo katika nafasi ya 12 na wanatakiwa washinde ili kujiondoka kwenye hatari yoyote ya kushuka daraja na kujiongezea matumaini ya kutafuta nafasi ndogo waliyonayo ya kushiriki michuano ya Ligi ya Europa, lakini Liverpool bado wanapambana kuingia ndani ya nne bora.

Pambano hili litachezeshwa na mwamuzi Muingereza, Antony Taylor. Katika mechi zake tano zilizopita, Liverpool imeshinda mbili, imetoa sare mbili na kupoteza moja, wakati Everton wameshinda mechi moja tu kati ya michezo yao mitano iliyopita huku mingine wakitoa sare.

Takwimu zinaonyesha kuwa, kwenye mechi tano zilizopita baina ya timu hizo, Liverpool imeshinda mara moja huku matokeo mengine yakibaki kuwa ni sare. Ngoma itakuwa pevu leo na lolote linaweza kutokea.

0 maoni:

Post a Comment