KATIBU Mkuu wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilbroad Slaa, amezitolea uvivu
klabu za Simba na Yanga kusema hazina jipya.
Slaa alitoa kauli hiyo
juzi Jumapili kwenye mkutano wa kumpongeza mwenyekiti mpya wa Serikali
ya Kibwegere, Edson Nyingi, uliofanyika kwenye viwanja vya Makombe,
Kibamba nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na umati
mkubwa wa wananchi waliojitokeza katika mkutano huo, Dk. Slaa alisema
kwa sababu Simba na Yanga zimeshindwa kufika popote, ni lazima zitafutwe
timu mbadala za kuweza kuchukua nafasi zao.
Alisema anasikitishwa
na klabu hizo kwani licha ya ukongwe zilionao katika Soka la Tanzania
zimeshindwa kuitangaza nchi kimataifa.
“Sina ugomvi na Simba
wala Yanga, lakini lazima tukubaliane kuwa zimeshindwa kuitangaza nchi
kimataifa na hii ni kutokana na mipango mibovu ya klabu hizi, hivyo ni
wakati wa vijana kujipanga kuanzisha timu zenye malengo.
“Angalia Azam, licha ya
kwamba ni timu changa iliyoanzishwa miaka ya hivi karibuni, lakini
imeonyesha dhamira ya dhati ya kuleta maendeleo ya soka kama
tunavyoshuhudia tayari wana uwanja wao,” alisema Dk. Slaa.
“Wana vitendea kazi
vingi na wapo wanazingatia soka la vijana lakini Simba na Yanga ziko
pale pale miaka nenda rudi, ni dhahiri kwa mwenendo huu hawatafika.”
0 maoni:
Post a Comment