Feb 3, 2015

HII INA MUHUSU FRANCIS CHEKA

Mke wa Cheka aangua kilio kortini

Bondia Francis Cheka akipanda kwenye gari ya polisi baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela. Picha na Mpigapicha Wetu 
Na Hamida Shariff na Imani Makongoro, Mwananchi

Posted  Jumanne,Februari3  2015  saa 14:15 PM
Kwa ufupi
Mumewe atupwa jela miaka mitatu, mashabiki, mabondia washikwa butwaa.
Morogoro/Dar . Wakati mke wa bondia maarufu nchini, Francis Cheka (32), Toshi Asenga akimwaga machozi mahakamani mumewe alipohukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na kulipa fidia ya Sh1 milioni, mabondia wa zamani, wadau wengine wameshikwa butwaa.
Katika hali ya kushangaza pamoja na umarufu wake, mashabiki wengi wa ngumi mjini Morogoro na vitongoji vyake hawakuwa na taarifa kuhusu kesi hiyo.

Cheka alitiwa hatiani kwa kosa la kumshambuliaji meneja wa baa yake, Bahati Kibanda.
Baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mke wa bondia huyo aliangua kilio akilalamika kuwa mumewe ameonewa na kwamba hakustahili kupewa adhabu hiyo kubwa.
Awali, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Cheka alitenda kosa hilo Julai 2 mwaka jana kwenye eneo la Ukumbi wa Vijana Social mjini Morogoro.

Ilidaiwa kuwa bondia huyo alimpiga ngumi na mateke maeneo ya tumboni na kichwani na hivyo kumsababishia Kibanda maumivu makali, wakati akijua kutenda hivyo ni kosa kisheria.
Akisoma hukumu, Hakimu Mkazi mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa wa Morogoro, Said Msuya alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambao haukuacha shaka yoyote katika kuthibitisha shtaka hilo.

“Adhabu hii itakuwa fundisho kwa mshtakiwa na watu wengine wanaotumia vibaya nguvu zao na mshtakiwa anatakiwa kumlipa fidia ya Sh1 milioni kwa mlalamikaji.”
Hata hivyo, Cheka alipopewa nafasi ya kujitetea aliieleza Mahakama kuwa hana maelezo yoyote zaidi ya kuiachia Mahakama iamue adhabu itakayompa.

Awali, mwendesha mashtaka wa Polisi, Anganile Nsiyani alidai mahakamani hapo na kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Julai 2 mwaka 2014 katika baa ya Vijana Social Hall iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Mwendesha mashtaka huyo alidai akijua kufanya hivyo ni kosa Cheka alimshambulia meneja wake wa baa (Bahati Kibanda) kwa kumpiga ngumi usoni na tumboni na hivyo kumsababishia maumivu makali.
Alipofikishwa Mahamani hapo kwa mara ya kwanza Cheka alikana shtaka hilo na hivyo upande wa mashtaka uliahidi kupeleka mashahidi wanne kati ya saba walioithibitisha mahakamani hapo bila ya shaka kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo na hivyo mahakama ikamtia hatiani.

0 maoni:

Post a Comment