Baada ya Simba kufungwa mabao 2-1 na Mbeya City, juzi Jumatano katika Ligi Kuu Bara,
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic, amefunguka kuhusu sababu zilizochangia kipigo
hicho huku akimtaja mchezaji mmoja kuhusika.
Kocha
huyo raia wa Serbia ametoa tamko juu ya mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa
Taifa kwa kusema kuwa kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wake, hasa Said Ndemla
kulisababisha upungufu mkubwa kwenye nafasi ya kiungo.
Ndemla
amepumzishwa kwa wiki mbili baada ya kuumia goti kwenye mechi yao dhidi ya Azam
FC.
“Tumefungwa
kihalali lakini kuna kitu pia nilikikosa kwenye timu yangu, Ndemla ni msaada
mkubwa sana, ni mchezaji niliyemuona mapema wakati natua kuifundisha Simba, ana
kila kitu kulingana na nafasi yake, kama angekuwepo sidhani kama tungepoteza
kirahisi kama ilivyokuwa.
“Ndemla
amebarikiwa sana, naweza kusema ni kipaji cha kipekee katika soka la Tanzania,
kama akiangaliwa kwa makini anaweza kuwa faida kubwa mno kwa taifa lake,
nimemkosa kwenye mechi, siwezi kusema kwamba angeitetea timu peke yake lakini
angekuwa na lolote la kutusaidia katika kutafuta ushindi.
“Sina
la kufanya, nitamsubiri apone lakini kila mchezaji ana ubora wake na sifa zake,
naweza kuwatumia wengine lakini Ndemla atabaki kuwa Ndemla kulingana na ubora
wake,” alisema Kopunovic.
0 maoni:
Post a Comment