MABINGWA wa kombe la Mapinduzi
2015, Simba SC kesho wanasaka pointi tatu kwa kila namna ili kupunguza
machungu waliyopata kwa kutandikwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City katika
mechi ya ligi kuu iliyopigwa juzi, januari 28 uwanja wa Taifa Dar es
salaam.
Simba watavaana na Maafande wa
JKT Ruvu Stars wanaonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Fredy Minziro,
katika mechi ya VPL itayopigwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Huu ni mtihani wa tatu kwa kocha
wa Simba SC, Goran Kopunovic kwani tayari ameshaiongoza timu hiyo katika
mechi mbili za ligi kuu.
Kopunovic alianza ligi kuu kwa
ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda fc, Januari 17 mwaka huu, kabla ya
kulazimisha sare ya 1-1 na Azam fc, Januari 24 mwaka huu. Juzi wakalala
2-1 dhidi ya Mbeya City.
Tayari baadhi ya wanachama na
mashabiki wa Simba wameanza chokochoko wakimtaka Rais wa Simba, Evans
Aveva ajiuzulu kutokana na kushindwa kuweka umoja katika klabu hiyo.
Aveva ambaye haamini kama mgogoro
wa Simba na wanachama wake wa UKAWA ndio chanzo cha kuboronga kwa timu,
amekaririwa mara kadhaa kuwa uongozi wake hauko tayari na hauna mpango
wa kukutana na kundi hilo maarufu nchini.
Lakini jana, Mwenyekiti wa kamati
ya usajili wa Simba, Zacharia Hans Poppe ambaye alifungua milango kwa
UKAWA kurudi klabuni kama watafuta kesi yao Mahakamani alisema wanasimba
hawana haja ya kuwalaumu viongozi kwa matokeo mabaya.
“Mchezaji kukosa penalti (Masoud
Nassor Cholo) unamlaumu vipi kiongozi. Labda yeye ndiye aulizwe
amekosaje penalti”. Alikaririwa Hans Poppe akiwatetea viongozi
kutohusika na matokeo hayo.
Hata hivyo alisema kuna haja ya kufanya uchunguzi ili kubaini kama kuna hujuma klabuni hapo.
Simba inakabiliwa na matokeo
mabaya ambapo mpaka sasa wameshinda mechi mbili tu dhidi ya Ruvu
Shootings na Ndanda fc katika mechi 11 walizocheza.
Wamefungwa mara mbili dhidi ya Kagera Sugar na Mbeya City na kutoka sare saba.
Tayari kocha Kopunovic ameshatoa kauli ya kuwakatisha tamaa Wanasimba kwamba wasahau kutwaa ubingwa mwaka huu.
Kocha huyo alisema kama Simba
wanawaza Ubingwa basi nayeye atafukuzwa kama ilivyotokea kwa makocha
wengine waliomtangulia kwani haamini kama ana kikosi cha Ubingwa.
Mpaka sasa Simba wapo nafasi ya 11 wakijikusanyia pointi 13 katika mechi 11 walizocheza.
0 maoni:
Post a Comment