BDF XI |
Kikosi cha timu ya BDF XI kimeshitukiwa kutokana na uamuzi wake wa kutangaza kutaka kujiondoa
katika michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga kwa madai ya ukata.
Ratiba
inaonyesha Yanga itaanza kuivaa BDF, Februari 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar.
Shirikisho
la Soka Afrika (Caf), limeingilia na kuonya kwamba BDF XI inachotakiwa ni
kuwasilisha barua mara moja kama kweli imejitoa badala ya kutumia suala hilo
kama mtego wa kuwababaisha wapinzani.
Caf
imesisitiza, iwapo BDF XI itajitoa basi itakumbana na adhabu ya kufungiwa
kutoshiriki michuano ya Caf kwa misimu miwili na faini ya dola 5,000 (Sh
milioni tisa).
Msemaji
wa BDF XI, Peo Keatlholetswe ameliambia Gazeti la Daily News la nchini humo
kwamba Caf imewapa onyo na kutaka kupata uhakika katika hilo.
“Tumeelezwa
kuwa tunatakiwa kutoa uhakika wa tunashiriki au la, wanaamini kusema bila
kuweka mambo wazi unaweza kuwa sawa na mchezo mchafu wa kutaka kuwababaisha
wapinzani wetu kutoka Tanzania.
“Tutaweka kila kitu wazi hivi karibuni,
lengo ni kujaribu kila namna ili tuweze kushiriki,” alisema Keatlholetswe.
Wakati
Keatlholetswe anaeleza kuhusiana na onyo hilo la Caf, benchi la ufundi la Yanga
limesema linajua mbinu zilivyo za kila aina, hivyo haliwezi kupunguza au
kuisimamisha programu yake ya maandalizi.
Bosi
msaidizi wa benchi la ufundi la Yanga, Charles Boniface Mkwasa, amefunguka
zaidi. “Tumesikia suala lao la kujitoa, lakini hatutasitisha jambo katika
programu yetu ya mazoezi. Tunachofanya ni kuendelea kama inavyotakiwa.
“Tutakuwa
makini maana timu inaweza kusema imejitoa kumbe inaendelea na maandalizi.
Michuano hii yenye ushindani mkubwa ina mbinu nyingi,” alisema Mkwasa ambaye
anaweza kuondoka siku yoyote kwenda Botswana kusoma mchezo wa wapinzani wao.
Hivi
karibuni Ligi Kuu ya Botswana ilipata bosi mpya wa bodi ya ligi ambaye amesema
BDF XI na mabingwa Township Rollers watakaoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika,
lazima wataiwakilisha Botswana.
Arnold
Somolokae amesema tayari juhudi za kuhakikisha Township Rollers inapata fedha
zake za ubingwa zimefanyika na sasa wanahangaika na BDF kuona inashiriki
michuano hiyo.
“Lazima
zishiriki, tayari tumeanza kampeni ya kuhamasisha watu zaidi kupenda soka.
Iwapo hazitashiriki haitakuwa na maana, tutapambana,” alisema.
0 maoni:
Post a Comment