Jan 30, 2015

NGASSA AELEZA KILICHOMFANYA ATOROKE KAMBINI YANGA



Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa, amesema kuwa amerejea kundini kuitumikia timu hiyo kwa moyo mmoja lakini kubwa zaidi ni kuwa anataka kuwaaga mashabiki wa Jangwani.


Tangu siku kumi zilizopita, Ngassa hakuonekana Jangwani huku Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Kiboroha akisikika akisema wamedokezwa kuwa staa huyo amekwenda Afrika Kusini kufanya majaribio lakini Ngassa mwenyewe amesema alitimkia Tanga kupumzisha akili kutokana na deni la shilingi milioni 45 analodaiwa na benki, ambalo amesusiwa na viongozi wa Yanga walilokubaliana walilipe kwa pamoja.

Ngassa ameliambia gazeti la maarufu la michezo nchini Tanzania la Championi kwamba amefikia maamuzi ya kurejea kwenye timu hiyo baada ya familia yake kuahidi kumsaidia kulipa deni hilo lililotokana na kiungo huyo kusaini Yanga akiwa ana mkataba na Simba.

Ngassa ambaye ameshajiunga na wenzake kambini Bagamoyo kujiandaa na mechi dhidi ya Ndanda FC itakayopigwa keshokutwa Jumapili, amesisitiza kuwa amepanga kujituma zaidi kuhakikisha Yanga inakuwa bingwa na kufanya vizuri kwenye mechi zote.

“Leo (juzi Jumatano) nimeingia kambini huku Bagamoyo nikiendelea na mazoezi kujiandaa na mechi ya ligi kuu dhidi ya Ndanda FC, hiyo ni baada ya familia yangu kuahidi kunisaidia kulipa deni langu la benki.

“Tumefikia hatua hiyo baada ya viongozi (wa Yanga) kukiuka makubaliano na kunisusia kulipa deni hilo, kiukweli akili yangu imerejea katika hali ya kawaida, hivyo ninaahidi kuitumikia timu yangu kwa moyo kwa kufunga na kutengeneza mabao kama njia ya kuwaaga mashabiki wa Yanga kutokana na mkataba wangu kumalizika mwisho wa msimu huu.

“Kikubwa ninataka kuwaonyeshea hao wanaozusha kuwa kiwango changu kinashuka kutokana na starehe na wanawake hao watatu wanaozusha nimewaoa wakati nina mke wangu mmoja wa ndoa,” alisema Ngassa.

0 maoni:

Post a Comment