Mar 16, 2015

SABABU ZA MRISHO NGASSA KULIA BADALA YA KUSHANGILIA MABAO YAKE JANA DHIDII YA PLATUMN

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MRISHO Khalfan Ngassa jana amefunga mabao mawili Yanga SC ikishinda 5-1 dhidi ya Platinum FC katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika, lakini hakushangilia badala yake akaanza kulia.
Kisa nini? Ngassa ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba alishindwa kuzuia hisia zake juu ya majonzi aliyonayo kufuatia kifo cha kocha Sylvester Marsh.
Marsh, kocha wa zamani wa timu za taifa, kuanzia za vijana, hadi ya wakubwa, Taifa Stars alifariki dunia juzi katika hospitali ya Muhimbili, Dar es Salaam alikokuwa amelazwa ya saratani ya koo.
Mwili wa Marsh uliagwa jana katika hospitali ya Muhimbili kabla ya kusafirishwa kwa basi dogo aina ya Coaster kupelekwa Mwanza kwa mazishi na Ngassa amesema msiba huo umemuumiza mno.
Mrisho Ngassa kulia akilia baada ya kufunga bao la nne katika ushindi wa Yanga SC wa 5-1
Ngassa kulia akilia baada ya kufunga bao la tano 

“Marsh amenifundisha mpira Kagera Sugar,lakini pia ndiye ambaye alinichukua kwa mara ya kwanza U17 (timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17,”.
Baada ya kufanya vizuri Serengeti ndipo milango ya mafanikio yangu kisoka ikafunguka, kwa hivyo unaweza kuona huyu ni mtu muhimu kiasi gani katika maisha yangu,”alisema Ngassa.
Nyota huyo wa timu ya Jangwani amesema kwamba baada ya kupata taarifa kwamba mwili wa Marsh utasifirishwa kwa basi, alijaribu kufanya jitihada za kuwezesha usafirishwe kwa ndege, lakini akakosa ushirikiano.
“Nilijaribu kuwatafuta ndugu za marehemu, lakini sikuwapata na bahati mbaya tulikua katika maandalizi ya mchezo wetu, hivyo nikakosa njia nyingine ya kufsnya. Ila msiba huu umeniumiza sana na nimeshindwa,”amesema.   
Ili Yanga isisonge mbele, inabidi ifungwe mabao 4-0 na Platinum katika mchezo wa marudiano wiki ijayo mjini Bulawayo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Djamaladen Aden Abdi, aliyesaidiwa na Hassan Eguech Yacin na Abdallah Mahamoud Iltireh wote wa Djibouti, hadi mapumziko, tayari Yanga SC walikuwa mbele kwa mabao 2-1.
Mabao ya Yanga SC yalifungwa na viungo Salum Abdul Telela ‘Master’ dakika ya 32 na Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ dakika ya 43, wakati bao la Platinum lilifungwa na Walter Musoma dakika ya 45.
Kipindi cha pili, Yanga waliongeza makali na kufanikiwa kupata mabao matatu zaidi, ambayo yanawafanya waende Bulawayo kwenye mchezo wa marudiano, wakiwa wana kazi ndogo tu.
Mabao hayo yalifungwa na Amisi Tambwe dakika ya 47 na Mrisho Ngassa mawili dakika ya 55 na 90.

0 maoni:

Post a Comment