SAMATTA ATUPIA GENK IKIUA 2-1

HII NDIO DROO KOMBE LA FA

SIMBA CHALII KESSY AONESHWA NYEKUNDU

MANARA APATA AJALI

MKENYA APIGA MBILI LIVERPOO IKIUA 4-1

Mar 14, 2015

OKWI AWAPA RAHA SIMBA SC, MTIBWA SUGAR AFA 1-0 TAIFA

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
BAO la Emmanuel Anord Okwi dakika ya 90 ushei limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni hii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba SC sasa inafikisha pointi 29 baada ya mechi 18 na kuendelea kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya mabingwa watetezi, Azam FC pointi 30 za mechi 16 sawa na vinara Yanga SC, wenye pointi 31.
Okwi alifunga bao hilo, wakati tayari baadhi ya wapenzi wa Simba SC wameanza kutoka uwanjani, wakiamni matokeo ni sare.  Mganda huyo, alifunga baada ya kupata pasi ya Abdi Banda na kumchambua vizuri kipa aliyefanya kazi nzuri leo, Said Mohamed Kasarama.

Wachezaji wa Simba SC wakimpongeza Okwi leo baada ya kufunga bao pekee la ushindi dakika za lala salama dhidi ya Mtibwa Sugar
Emmenuel Okwi akimtoka beki wa Mtibwa Sugar, Said Mkopi katika mchezo wa leo

Beki wa Simba SC, Hassan Kessy akimtoka kiungo wa Mtibwa Sugar, Shaaban Nditi 
Mchezo huo uliochezeshwa na refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga, aliyesaidiwa na Yussuf Sekile wa Ruvuma na Abdallah Rashid wa Pwani, Simba SC ndiyo waliotawala na kutengeneza nafasi nyingi, lakini hawakuwa na bahati ya mapema.
Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi aliiongoza vyema safu ya ushambuliaji ya Mtibwa Sugar akisaidiana na Ame Ally, lakini wakaishia kuisumbua tu ngombe ya Simba, iliyoongozwa na beki chipukizi, Hassan Isihaka.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Said Ndemla, Abdi Banda, Elias Maguri, Emmanuel Okwi na Simon Sserunkuma/Ramadhani Singano ‘Messi’. 
Mtibwa Sugar; Said Mohammed, Said Mkopi, Dacis Luhende, Salim Mbonde, Andrew Chikupe, Shaaban Nditi, Ally Sharrif, Henry Joseph, Ame Ally/Mohammed Mkopi, Muzamil Selemba/Ally Yussuf na Mussa Hassan Mgosi/Vincent Barnabas.  


UKIKUTWA NA TIKETI FEKI YA YANGA NA PLATINUM KESHO TAIFA, UMEKWISHA!

Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
YANGA SC imeonya, atakayekamatwa na tiketi feki za mchezo wao na Platinum FC kesho ‘amekwisha’.
Yanga SC wanaikaribisha Platinum FC ya Zimbabwe kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
Na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro amesema wamechapisha tiketi za kiwango cha juu, ambazo si rahisi mtu ‘kufoji’ akapatia kila kitu.

“Sasa atakayethubutu kufoji na sisi tukamnasa kwa kweli amekwisha,”amesema. Muro amewaasa mashabiki kununua tiketi katika sehemu zilizotajwa, ili kuepuka kununua feki.
Kiingilio cha chini kitakuwa na Sh. 5,000 kwa jukwaa la viti vya rangi bluu na kijani, wakati katika jukwaa la viti vya Rangi Chungwa itakuwa Sh, 10,000, VIP C Sh. 20,000, VIP B Sh. 25,000, na VIP A Sh 30,000.
Muro amesema tiketi zimeanza kuuzwa leo asubuhi katika vituo vya Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Aidha, amesema magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya Uwanja siku ya Jumapili.
Yanga SC imefika hatua hii baada ya kuitoa BDF XI ya Botswana, wakati Platinum iliing’oa Sofapaka ya Kenya.

MARSH KUAGWA JUMATATU KARUME, MAZISHI MWANZA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MWILI wa aliyekuwa kocha Msaidizi wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Sylvester Marsh utaagwa Jumatatu kuanzia Saa 4:00 asubuhi Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa Mwanza kwa mazishi.
Mtoto wa kaka wa marehemu Marsh, aitwaye Abdallah Ramadhani, ambaye alikuwa anamuuguza baba yake mdogo amesema taratibu za mazishi zinaendelea.  
Marsh amefariki dunia Alfajiri ya leo katika hospitali ya Muhimbili alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya saratani ya koo.
Na ilielezwa, Marsh alikuwa amekuja Muhimbili kuhudhuria kliniki yake ya kawaida juu ya maradhi ya saratani ya koo yanayomsumbua na ghafla hali yake ikabadilika juzi hadi kufariki dunia.
Sylvester Marsh (katikati) enzi za uhai wake akiwa Jacob MIchelsen kulia na Kim Poulsen kushoto

Marsh alianza kuwa Kocha Msaidizi wa timu za vijana Tanzania mwaka 2003 chini ya Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ kabla ya mwaka 2006 kupandishwa timu ya wakubwa, akianza kumsaidia Mbrazil, Marcio Maximo na baadaye Wadenmark, Jan Poulsen na Kim Poulsen.
Hata hivyo, baada ya Jamal Malinzi kushinda Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Oktoba mwaka juzi, alibadilisha benchi zima la ufundi la Taifa Stars na Marsh akaondoka pamoja na Kim Poulsen. Sasa Mholanzi, Mart Nooij ndiye kocha Stars, anasaidiwa na Salum Mayanga.
Tangu hapo Marsh amerudi kufanya kazi katika kituo chake cha Marsh Academy mjini Mwanza, lakini mwaka jana ndipo maradhi ya saratani koo yalipoibuka na akaletwa Muhimbili kwa matibabu.
Mfanyabiashara Abdulfatah Salim, mmiliki wa hoteli ya Sapphire Court, alimsaidia kocha huyo hadi akafanyiwa upasuaji na hali yake kuimarika Februari mwaka jana na kurejea Mwanza.
Marsh alipata ahueni ya kutosha na kuanza tena kazi ya kufundisha watoto wake wa Marsh Academy, kabla ya wiki hii kuletwa Dar es Salaam kuhudhuria kliniki.
Mbali na timu za taifa, Marsh pia amefundisha klabu za Toto Africans ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Azam FC ya Dar es Salaam.
Miongoni mwa mafanikio yake akiwa kocha, mwaka 2005 aliiwezesha Kagera Sugar kutwaa Kombe la Tusker, ikiifunga Simba SC katika fainali mabao 2-1 Dar es Salaam.
Mwaka 2004, akiwa Msaidizi wa Kibadeni katika U17, maarufu Serengeti Boys, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika nchini Gambia, baada ya kuzitoa Rwanda, Zambia na Zimbabwe. 
Hata hivyo, timu hiyo iliyoibua vipaji vya wachezaji waliogeuka nyota wa taifa kwa miaka 10 iliyopita kama Nizar Khalfan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Amir Maftah na wengine, ilienguliwa fainali za Gambia kwa kashfa ya kumtumia Nurdin Bakari aliyekuwa amezidi umri.
Mwaka 2009, Marsh akiwa Msaidizi wa Maximo Taifa Stars, waliiwezesha timu hiyo kukata tiketi ya kucheza fainali za kwanza za CHAN nchini Ivory Coast.
Inaelezwa kwa muda wote wa Marsh kufanya kazi na timu za taifa hakuwahi kuwa na Mkataba, bali alikuwa kama ‘deiwaka’ maana yake hakuweka mbele maslahi, bali uzalendo. 
Bwana ametoa, bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe. Mbele yake, nyuma yetu. Mungu ampumzishe kwa amani mwalimu Sylvester Marsh. Amina. 

SIMBA UKAWA WAKUBALI KUISHANGILIA YANGA, LAKINI KWA MASHARTI HAYA...



Baada ya uongozi wa Yanga kuwaomba mashabiki wa klabu tofauti za hapa nchini kujitokeza na kuwapa sapoti kwenye mchezo wao wa kesho Jumapili wa Kombe la Shirikisho dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe, mashabiki wa Simba wa Tawi la Mpira na Maendeleo, maarufu kwa jina la Simba Ukawa, wamekubali kufanya hivyo ila wakatoa masharti.

Yanga, kesho inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, kucheza na Platinum, mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya michuano hiyo. Ikumbukwe kuwa Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuiondoa BDF IX ya Botswana, huku wapinzani wao wakiitoa Sofapaka ya Kenya.

Mwenyekiti wa tawi hilo, Mohammed Kingolile, amesema kuwa wao linapokuja suala la klabu kuiwakilisha nchi, huwa hawana kinyongo na Yanga, hivyo wapo tayari kuishangilia kwa nguvu zote.

“Tupo tayari kuwashangilia lakini kauli za kuikejeli Simba alizozitoa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa timu yao, Jerry Muro, kabla ya mchezo wetu dhidi yao wiki iliyopita, zimetufanya kusita kuishangilia mpaka pale watakapotuomba radhi.”

SOURCE: CHAMPIONI JUMAMOSI.

MIKATABA YA NIYONZIMA, NGASSA YAMALIZIKA YANGA, WAKO HURU KWENDA ZAO

NGASSA (KULIA....
Viungo wa Yanga Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na Mrisho Ngassa wamesema, mikataba yao imekwisha na wanawaaga kabisa mashabiki wao.

Viungo hao, kila mmoja ameaga kuondoka kwa sababu tofauti huku ikikumbukwa kuwa mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.

Kauli hiyo, imetolewa na viungo hao ikiwa ni siku chache tangu kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba ambayo ilimalizika kwa Yanga kufungwa bao 1-0 kabla ya tuhuma za hujuma kwa wachezaji wa timu hiyo kutolewa na mashabiki.
Niyonzima amesema kuwa imetosha kuichezea Yanga, hivyo ameona bora aondoke na kuwaachia mashabiki timu yao huku akiitakia mafanikio.
 
NIYONZIMA (KULIA)...
Niyonzima alisema, kichwa chake hakipo vizuri, hivyo anahitaji muda zaidi wa kupumzisha akili yake kwa kutoongeza mkataba mwingine na kurudi kwao Rwanda.
Mrwanda huyo alisema amechoshwa na kashfa anazoendelea kupewa na baadhi ya viongozi na mashabiki wa Yanga kuhusiana na kuihujumu kwenye mechi dhidi ya Simba.
“Nilikuwa tayari kuongeza mkataba mwingine wa kuichezea Yanga baada ya hivi karibuni kufanya mazungumzo na viongozi, lakini nimesitisha mpango huo hivi sasa na badala yake nitarudi zangu nyumbani kupumzika.
“Kiukweli nimechoshwa na taarifa za mimi kila tunapokutana na Simba ninacheza chini ya kiwango, mechi ya mwisho tuliyocheza na Simba wiki iliyopita mengi yaliongelewa na baadhi ya viongozi na mashabiki kuwa nimeihujumu timu kwa kucheza chini ya kiwango, kitu ambacho siyo kweli.
“Hivyo sitasaini tena Yanga na badala yake nitarudi zangu Rwanda kupumzisha akili yangu, pia sipo tayari kuichezea timu yoyote ya hapa nchini, kwa sababu matatizo yaliyopo Yanga yapo huko pia,” alisema Niyonzima.
Kwa upande wa Ngassa yeye alisema: “Mimi sasa hivi akili yangu inafikiria kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi na siyo hapa nchini, zipo tetesi nyingi zinazozungumza kuwa nimesaini Simba mara Azam FC.


“Ukweli ni kwamba hiki ndiyo kipindi changu muafaka kwa mimi kuondoka Yanga, ninataka mafanikio zaidi, ninaondoka Yanga bila ya kinyongo na mtu, niliipenda timu yangu ya Yanga lakini sitarajii kuongeza mkataba,” alisema Ngassa.

SOURCE: CHAMPIONI JUMAMOSI

MDAU ABDULFATAH WA SAPPHIRE AMLILIA KOCHA MARSH

Mdau maarufu wa soka nchini, Abdulfatah Saleh ameeleza hisia zake kwa kusikitishwa na msiba ulioikumba familia ya wanamichezo na hasa wapenda soka baada ya kuondokewa na Sylvester Marsh.


Marsh aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars, Kilimanjaro Stars na baadhi ya timu za Ligi Kuu Bara, amefariki leo asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Marsh alilazwa Muhimbili wiki chache zilizopita akisumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya koo ambao ulikuwa ukimsumbua kwa muda sasa.

Kumbukumbu zinaonyesha mdau huyo alikuwa kati ya waliojitokeza kumsaidia Marsh kwa hali na mali wakati akiwa mgonjwa.

Abdulfatah, mmiliki wa Hoteli ya Sapphire Court ya Kariakoo jijini Dar es Salaam alisema msiba wa Marsh ni sehemu ya mafunzo kwa wanamichezo kama wanadamu.

"Kila mmoja ataonja mauti, hili ni vizuri kila mmoja kulikumbuka. Lakini tujifunze pia kusaidiana na kupendana wakati tukiwa hai.

"Urafiki si kufanana, ni kufaana. Vizuri mtu anapokuwa na matatizo tukamkumbuka kwa kuwa hatujui baada ya fulani, matatizo yatahamia kwa nani," alisema Abdulfatah akionyeshwa kuguswa na msiba wa kocha huyo aliyekuwa akimiliki kituo cha kukuza vipaji vya watoto katika mchezo wa soka huko Mkoani Mwanza.

Ingawa alikuwa akifanya siri kubwa huenda kwa kufuata misingi ya dini, Abdulfatah ndiye alijitolea kumhudumia kocha huyo katika matibabu yake.


Juhudi kuhakikisha Marsh anapata matibabu bora hadi alipopata nafuu na kurejea kwao Mwanza. Lakini baada ya miezi michache baadaye alirejeshwa tena akiwa katika ambayo haikuwa nzuri hadi mauti yalipomkuta.

UNAMKUMBUKA BOBAN, ANGALIA BINSLUM ALICHO MFANYA

Mmoja wa viungo wenye uwezo wa juu ni Haruna Moshi ‘Boban’. Lakini siku hizi ameadimika na amekuwa akifanya mazoezi binafsi.

Mmoja wa wadau wa soka na kiongozi wa Villa Squad, Iddi Godigodi ametupia picha Boban akijaribu kumdhibiti mshambuliaji ‘hatari’ Nassor Bin Slum.
Katika picha hiyo ya mtandao wa kijamii aliyotupia Godigodi, inaonekana Boban akijaribu kumba Bin Slum akiwa kwenye mwendo.

Fitness ya Bin Slum inaonekana kuwa juu na Boban anayumba akiwa njiani kuelekea kulamba mchanga.
Walioiona picha hiyo, maswali yao” Huyu huyu Bin Slum anayezidhamini Mbeya City, Stand  United na Wana Ndanda kucheeree yuko fiti hivi”.
Wengine: “Boban kwa ameisha kiasi hicho?” basi kila mmoja ana swali lake.

Lakini ukweli katika picha unaonyesha Boban amezidiwa na mshambuliaji huyo ambaye alikuwa majeruhi, sasa amerejea dimbani.

KURASA ZA MWANZO NA ZA MWISHO ZA MAGAZETI YA LEO ZIPO HAPA MARCH 14

.
.
.
.
.
.
.
.
.
DSC00551 DSC00552

WAKURUGENZI AZAM FC WAPATA ‘LANCHI’ NA WACHEZAJI, WAPANGA NAO MIKAKATI YA KUTETEA UBINGWA

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
WAKURUGENZI wa klabu ya Azam FC, leo wamesali pamoja na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo sala ya Ijumaa kabla ya kupata nao chakula cha mchana wachezaji wote.
Hiyo ilikuwa kabla ya kikao maalum cha kuweka mikakati ya kuhakikisha timu inatetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kilichofanyika Mikocheni, Dar es Salaam, nyumbani kwa Yussuf Bakhresa, mmoja wa Wakurugenzi.
Pamoja na Yussuf, alikuwepo Omar Bakhresa, wote watoto wa bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa, na mdogo wake, Jamal Bakhresa.
Yussuf Bakhresa akizungumza na wachezaji leo nyumbani kwake, Mikocheni, Dar es Salaam
Jamal Bakhresa kulia na Omar Bakhresa kushoto wakichukua chakula
Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa 'Father' kulia akiwa na Omar Bakhresa 

Wakurugenzi hao walianza kwa kuwapongeza wachezaji kwa kuifikisha timu ilipo sasa na wakawaambia hawajasononeshwa na kutolewa kwao katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Azam FC ilitolewa na El Merreikh ya Sudan katika Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikifungwa 3-0 ugenini baada ya kushinda 2-0 nyumbani.
Baada ya hapo, uongozi ulimfukuza kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog na msaidizi wake namba mbili, Mkenya Ibrahim Shikanda na timu kwa sasa ipo chini ya Mganda, George ‘Best’ Nsimbe.
Juzi, bodi ya Ukurugenzi imemuongeza aliyekuwa kocha wa Ndanda FC, Dennis Kitambi kuwa Msaidizi wa Nsimbe kwa muda.
Katika kikao hicho, Omar Bakhresa aliwaambia wachezaji kwamba wao hawajasononeshwa na matokeo ya timu kutolewa mapema Ligi ya Mabingwa kwa sababu wanafahamu hiyo ndiyo soka.
“Timu kama Manchester City, inawekeza fedha nyingi mno, inasajili wachezaji wakubwa duniani, lakini bado haijaweza kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Ulaya,”.
“Sasa na sisi tunajua ni suala la wakati tu, wakati ukifika Azam itakuwa bingwa wa Afrika, hizo ndizo ndoto zetu na ndiyo maana hatuchoki kuwekeza kila siku,”alisema.
Yussuf Bakhresa kwa upande wake aliwaambia kwamba wachezaji hawatakiwi kujisikia unyonge kwa kutolewa mapema kwa sababu hayo ni matokeo ya kawaida katika soka.
“Sisi tuliona, mlipambana kadiri ya uwezo wenu. Kwanza tunawapongeza hata kuwafunga 2-0 hapa nyumbani, halikuwa jambo jepesi. Tunaomba msife moyo, huo si mwisho. Jitahidini mtetee ubingwa wa Ligi Kuu, ili mwakani muende mkasahihishe makosa yenu,”alisema.
Yussuf amewataka wachezaji wao kwa wao kushikamana, kupendana na kucheza kwa ari kuhakikisha wanachukua tena ubingwa wa Ligi Kuu.
“Yanga wanatuzidi pointi moja. Hii maana yake tunapaswa kushinda mechi zetu zote zilizobaki ikiwemo mechi yetu dhidi yao, ili tuwe mabingwa. Hii si kazi nyepesi, lakini kwa sababu tunaamini uwezo wenu, tunaamini inawezekana,”alisema Yussuf.
Yussuf aliwaambia nia ya Bodi ya Ukurugenzi ipo pale pale, ni kuifanya Azam FC iwe klabu kubwa Afrika na mikakati zaidi ya kuboresha mfumo wa uendeshwaji inakuja.
“Siku si nyingi, mtasikia mambo makubwa sana hapa Azam, itakuwa klabu ya kipekee Afrika. Sitaki kuwaambieni kila kitu, ila vuteni subira mtasikia,”alisema.
Naye Jamal Bakhresa, aliwaambia wachezaji waongeze juhudi kwa sababu sasa ushindani ni mkubwa katika Ligi Kuu.
Wachezaji wa Azam FC wakichukua chakula nyumbani kwa bosi wao jana
Jamal Bakhresa (kushoto) akizungumza huku Yussuf Bakhresa (kulia) na Kipre Tchetche (katikati) wakisikiliza
Wachezaji wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba kulia na Erasto Nyoni kushoto jana kwa 'bosi Yussuf' mchana

“Simba SC wanakuja, wapo nyuma yetu. Nao wanataka nafasi. Kwa hiyo mnatakiwa kucheza kila mechi kama fainali, ligi ipo ukingoni hii. Sasa hivi kila timu itawakamieni, lakini ni wanaume wenzetu hao, pambaneni na muwafunge,”alisema. 
Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliwashukuru Wakurugenzi kwa kuonyesha wanawajali na akaahidi wanakwenda kupambana kuhakikisha wanatetea ubingwa.
“Sisi tunashukuru sana, hii mmeonyesha mnatujali na nyinyi ni watu wa michezo kweli. Kweli tulisikitishwa baada ya kutolewa na El Marreikh, kwa sababu dhamira yetu ilikuwa ni kufika mbali,”
“Lakini tunasema hayo yote tunayaacha nyuma, na sasa tunaelekeza nguvu katika kutetea ubingwa,”alisema Bocco.   
Kwa sasa katika msimamo wa Ligi Kuu, Azam FC inashika nafasi ya pili kwa pointi zake 30, nyuma ya Yanga SC, yenye pointi 31, baada ya kila timu kucheza mechi 16. Simba SC yenye pointi 26 ni ya tatu baada ya kucheza mechi 17.
Wakati Azam FC itashuka tena dimbani Jumatatu kumenyana na Ndanda FC, Simba SC wao watamenyana na Mtibwa Sugar kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga SC keshokutwa itameyana na Platinum FC ya Zimbabwe katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya katikati ya wiki kukipiga na JKT Ruvu katika Ligi Kuu.    

PLATINUM WATUA DAR, WAJICHIMBIA POSTA

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KIKOSI cha Platinum FC kimewasili usiku huu Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Yanga SC Jumapili.
Msafara wa watu 31 wakiwemo wachezaji na viongozi ulitua ardhi ya Dar es Salaam Saa 3:30 usiku wa Ijumaa na kupokewa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga SC, Jerry Muro.
Mara baada ya kuwasili, msafara huo ulielekea katika hoteli ya Tifanny, eneo la Posta mjini Dar es Salaam kwa basi dogo walilotayarishiwa na wenyeji wao hao.
Wachezaji wa Platinum baada ya kuwasili Dar es Salaam
Wachezaji wa Platinum wakisubiri taratibu za Uhamiaji zikamilike ili waingia Dar es Salaam
Jerry Muro ndiye aliyewapokea
Wachezaji wa Platinum wakipanda basi walilotayarishiwa  na wenyeji wao, Yanga SC

Kikosi hicho, Jumamosi kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Saa 3:00 asubuhi, wakati jioni watawapisha wenyeji wao, Yanga SC.
Maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na kiingilio cha chini kitakuwa na Sh. 5,000 kwa jukwaa la viti vya rangi bluu na kijani.
Muro aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, katika jukwaa la viti vya Rangi Chungwa itakuwa Sh, 7,000, VIP C Sh. 15,000, VIP B Sh. 20,000, na VIP A Sh 30,000.
Muro amesema tiketi zitaanza kuuzwa Jumamosi Saa 2:00 asubuhi katika vituo vya Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Aidha, amesema magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya Uwanja siku ya Jumapili.
Yanga SC imefika hatua hii baada ya kuitoa BDF XI ya Botswana, wakati Platinum iliing’oa Sofapaka ya Kenya.