SAMATTA ATUPIA GENK IKIUA 2-1

HII NDIO DROO KOMBE LA FA

SIMBA CHALII KESSY AONESHWA NYEKUNDU

MANARA APATA AJALI

MKENYA APIGA MBILI LIVERPOO IKIUA 4-1

Mar 17, 2015

HUKUMU MPYA YA BONDIA FRANCIS CHEKA


francUnakumbuka ile skendo iliyompata bondia wa ngumi nchini Francis Cheka baada ya kumpiga na kumuumiza meneja wa baa yake akimtuhumu kusababisha hasara?
Taarifa iliyotolewa na kocha wake Abdalah Komando na kuthibitishwa na wanafamilia yake inasema Bondia huyo nyota zaidi nchini sasa ameachiwa huru na atakuwa akitumikia kifungo cha nje.
Alisema Cheka ameachiwa huru baada ya kushinda rufaa yake aliyokata kupinga kifungo cha miaka mitatu gerezani na sasa anatumikia kifungo cha nje.
Tayari Cheka alianza kutumikia kifungo hicho mjini Morogoro lakini taarifa za uhakika zinasema ameachiwa leo baada ya kushinda rufaa hiyo.
“Tayari ameachiwa, Ila tayari yuko nje, tunashukuru kwa hatua hii lakini bado kesi yake inaendelea kwa kipindi chote cha miaka mitatu” alisema kocha wake Abdalah Komando
Cheka alihukumiwa kwenda jela baada ya kumuumiza meneja wa baa yake mjini Morogoro akimtuhumu kumsababishia hasara katika baa yake.

TWIGA STARS KUWAFUATA ZAMBIA IJUMAA

Na Baraka Kizuguto, DAR ES SALAAM
MSAFARA wa watu 25 wa timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars), unatarajiwa kuondoka nchini siku ya ijumaa kuelekea nchini Zambia kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia siku ya jumapili.
Twiga Stars inaanzia hatua ya pili katika kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa Wanawake baada ya kuwa katika nafasi za juu kwa viwango barani Afrika, na endapo itafanikiwa kuwaondoa Wazambia itafuzu moja kwa moja kwa fainali hizo.
Wachezaji wa Twiga Stars wakiwa mazoezini hivi karibuni

Msafara utaongozwa na Blassy Kiondo (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji), Beatrice Mgaya (kiongozi msaidizi), Rogasin Kaijage (kocha mkuu), Nasra Juma (kocha msaidizi), Furaha Francis (Meneja), Christine Luambano (Daktari) na Mwanahamis Abdallah (Mtunza vifaa).
Wachezaji watakokweda Zambia ni Asha Rashid, Mwajuma Abdallah, Mwanahamis Omar, Donisi Minja, Amina Bilal, Fatuma Bashiri, Esther Chabruma, Shelda Mafuru, Maimuna Kaimu, Najiat Abbas, Stumai Abdalla, Fauma Issa, Thereza Yona, Fatuma Hassan, Fatuma Omary, Sophia Mwasikili, Fatuma Khatibu na Etoe Mlenzi.

HAYA NDIO MAPATO YANGA VS PLATINUM

Na Baraka Kizuguto, DAR ES SALAAM
MECHI ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya timu ya FC Platinum ya Zimbambwe iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam iliingiza mil 91,660,000 kutokana na watazamaji 14,563 waliokata tiketi kushuhudia mchezo huo.
Mgawanyo wa mapato katika mchezo huo ni, VAT 18% sh. 13,982,033, Gharama ya tiketi sh. 12,380,000, Uwanja 15% sh. 9,794,694.92, Gharama za mchezo 15% sh. 9,794,694.92, TFF 5% sh. 3,264,898.31, CAF 5% sh. 3,264,898.31 na Young Africans 60% sh.39.178,779.66.
Katika mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo, Yanga SC ilianza kwa ushindi wa 5-1 nyumbani dhidi ya Platinum FC na sasa itakwenda kupigania hata sare ugenini wiki ijayo ili kusonga mbele.
Salum Telela akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza katika ushindi wa 5-1 dhidi ya Platinum Jumapili

PLUIJM ASEMA SUALA LA DHARAU HALITAKUWEPO WAKITUA ZIMBABWE


Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm amesema pamoja na ushindi wa mabao 5-1, kamwe hawatatanguliza dharau watakapokuwa ugenini dhidi ya FC Platinum ya Zimbabwe.

Pluijm raia wa Uholanzi amesema timu nyingi dunia zimewahi kuanguka licha ya kuwa zilitangulia kupata ushindi mnono kwa sababu ya dharau.
“Unaweza kusema sisi ndiyo tunaopaswa kuwa makini zaidi hata kuliko wao. Kweli tumeshinda tano nyumbani, lakini tuna uhakika gani wao hawawezi kushinda.
“Lazima tuamini kupita kwetu kutahakikishwa na mechi ya pili. Dakika 90 bado hatuazimaliza.

“Nimezungumza na wachezaji lakini hili nitaendelea kulikumbusha tena na tena,” alisema Pluijm.


Yanga ilionyesha kiwango cha juu katika mechi hiyo Jumapili na kufanikiwa kuwaangusha Wazimabwe hao kwa kipigo cha hatari.

ETOILE DU SAHEL WABISHA HODI YANGA SC, ILA KUNA WAANGOLA HATARI NAO!

Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
ETOILE du Sahel ya Tunisia imejiweka katika mazingira magumu ya kwenda 16 Bora ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika baada ya jana kushinda 1-0 nyumbani dhidi ya S.L. Benfica ya Angola.
Ikumbukwe mshindi wa jumla baina ya timu hizo mbili, ndiye anaweza kukutana na Yanga SC ya Tanzania, ambayo jana ilianza na ushindi wa 5-1 nyumbani dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe.
Sasa Etoile, timu ya zamani ya mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, Emmanuel Okwi ambaye kwa sasa yupo Simba SC ya Tanzania pia, inatakiwa kwenda kulazimisha sare na Sport Luanda de Benfica nchini Angola ili kufuzu.
Etoile du Sahel jana wameshinda 1-0 nyumbani 
Benfica de Angola ni timu yenye rekodi nzuri ya kushinda nyumbani Luanda

Au ifungwe kwa tofauti ya bao moja kuanzia 2-1, 3-2 ndipo ifuzu kwa faida ya mabao ya ugenini.
Wakati Etoile imeanzia Raundi ya kwanza katika michuano hii, Benfica de Luanda iliitoa Le Messager Nzogi ya Burundi katika Raundi ya Awali kwa jumla ya mabao 3-0, ikianza kushinda nyumbani 2-0 kabla kwenda kushinda 1-0 na Bujumbura.
Lakini tayari inaelezwa kwamba Benfica ni timu yenye rekodi nzuri ya ushindi katika mechi za nyumbani Uwanja wa 11 de Novembro mjini Luanda.
Yeyote atakayesonga mbele, dhahiri Yanga SC itakutana na mpinzani mgumu katika hatua inayofuata iwapo itafanikiwa kufuzu. 
Kihistoria, mpinzani kutoka Kusini mwa Afrika atakuwa nafuu kwa Yanga SC, kuliko Kaskazini. Yanga SC haijawahi kuitoa timu ya Kaskazini mwa Afrika katika mashindano ya Afrika, lakini imewahi kuzitoa timu za Kusini mwa Afrika, ikiwemo Angola.  
Mara ya mwisho Yanga SC ilikutana na Petro Atletico ya Angola mwaka 2007 na ikaitoa kwa jumla ya mabao 3-2, ikianza kushinda nyumbani 3-0 kabla ya kwenda kufungwa ugenini 2-0.

COASTAL UNION WAIKAMIA AZAM FC

Na Mwandishi Wetu, TANGA
TIMU ya Coastal Union imewasilia jijini Tanga ikiwa na mikakati mizito ya kuhakikisha inawanyamazisha wapinzani wao Azam FC ikiwa ni muendelezo wa Michuano ya Ligi kuu soka Tanzania bara mchezo unaotarajiwa kucheza kwenye uwanja wa CCM Mkwakwani wikiendi ijayo.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Ofisa Habari wa Coastal Union, Oscar Assenga amesema kuwa sasa nguvu zao watazielekeza kwenye mchezo huo utakaochezwa kwenye mjini hapa.
Coastal Union wakiwa mazoezini mjini Tanga leo

Amesema kuwa dhamira yake aliyoipanga ni kuchukua pointi tatu muhimu dhidi ya Ruvu Shooting haikuweza kutimia na kujikuta wakilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 hivyo atahakikisha inatimia kwenye mechi hiyo.
Amesema timu hiyo imerudi salama mkoani hapa na tayari wameshaanza kujipanga imara kuhakikisha mechi hiyo timu inapata ushindi n kutokana na uimara wa kikosi chao
Aidha amesema kuwa wachezaji wa kikosi hicho wameimarika zaidi na wapo imara kuweza kupambana kufa na kupona ili kuchukua pointi tatu muhimuzo zitawasogeza kwenye nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi hiyo.
Hata hiyo amewataka wapenzi na mashabiki wa soka mkoani hapa kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika mchezo huo ili kuipa hamasa timu hiyo kuweza kutimiza ndoto zake.

SHERMAN AWAAMBIA YANGA WAMPE MUDA, WATAFURAHI NA ROHO ZAO

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI Mliberia wa Yanga SC, Kpah Sean Sherman amewaomba mashabiki wa timu hiyo kumsapoti na kumpa muda, akiamini siku moja ataanza kuwafurahisha.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini Dar es Salaam, Sherman alisema kwamba anafahamu kiu ya mashabiki wa timu hiyo ni kumuona anafunga mabao na kuisaidia timu kufanya vizuri.
“Mimi ni mchezaji mzuri na ambaye najiamini. Mimi ni mshambuliaji halisi. Mimi ni mfungaji asilia. Bado sijaonyesha yote hayo hapa Yanga, lakini naamini wakati ukifika nitaonyesha,”alisema.
Kpah Sherman akiibusu nembo ya Yanga juzi kuashiria ana mapenzi na klabu hiyo
Sherman akiwapa ishara ya "Suala la muda" mashabiki wa Yanga juzi

Sherman alisema kwamba mwanzoni hali ya kukosa mabao ilimsababishia msongo wa mawazo hadi akajikuta anashindwa hata kucheza vizuri, lakini alipoamua kuikubali angalau anaanza kurudi kucheza katika kiwango chake.
Sherman alitokea benchi juzi katikati ya kipindi cha pili na kwenda kutoa pasi ya bao la tano, Yanga SC ikishinda 5-1 dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe katika mchezo wa kwanza, Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.
Na baada ya kutoa pasi hiyo ya bao, lililofungwa na Mrisho Ngassa, Sherman alikimbilia mbele ya jukwaa la mashabiki wa Yanga na kubusu nembo ya timu, huku akionyesha ishara ya kugusa saa, kumaanisha “Ni suala la muda”.
Sherman ameiambia BIN ZUBEIRY;  “Kufunga mabao ni suala la muda tu, ukifika nitafunga tena sana, mashabiki wa Yanga lazima wajifunze kuwa na wachezaji wao. Wao wasiwakatishe tamaa wachezaji wao, hiyo kazi wawaachie Simba,”alisema.
Amesema yeye ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa na hakuna shaka juu ya hilo, kikubwa anachoomba mashabiki wa Yanga wajenge imani juu yake na kumsapoti.
“Natakiwa nijivunie mashabiki wa timu yangu, wao wanatakiwa kunitia moyo. Wasinikatishe tamaa. Mimi nina uwezo, sibahatishi,”amesema mchezaji huyo aliyesajiliwa Desemba kutoka Cyprus alipokuwa anacheza soka ya kulipwa.