Kiungo wa
timu ya Coastal Union, John Mahundi amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi
Disemba 2014 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea kutimua vumbi kwenye
viwanja mbalimbali nchini.
Mahundi
alitoa mchango mkubwa kwa timu yake ya Coastal Union mwezi Disemba mwaka jana
na kuchaguliwa na jopo la makocha linalofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora wa
kila mwezi.
Aidha
mshambuliaji wa timu ya Polisi Morogoro, Said Bahanuzi amechaguliwa kuwa
mchezaji bora mwezi Januari 2015 wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inayoendelea
kutimua vumbi mzunguko wa 15 kwenye viwanja mbalimbali nchini.
Bahanuzi
anayechezea timu ya Polisi Morogoro kwa mkopo akitokea timu ya Young Africans
amekua na mchango mkubwa kwa timu yake tangu kujiunga nayo mzunguko wa pili wa
Ligi Kuu ya Vodacom nchini.
Kwa kuibuka
wachezaji bora, Mahundi na Bahanuzi watazawadiwa fedha taslimu sh. milioni moja
kwa kila mmoja kutoka kwa wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom.
Jopo maalumu la makocha waliopo katika viwanja vyote vinavyotumika kwa mechi za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ndiyo wanaofanya kazi ya kuchagua mchezaji bora kwa kila mechi kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa, na baadaye alama zao kujumlishwa ili kumpata mshindi wa mwezi.
0 maoni:
Post a Comment